CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Ukonga kimezidi kujiimarisha kwa kuzindua matawi ya msingi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, mkakati unaokwenda sambamba na uchaguzi wa viongozi.
Uzinduzi huo ambao unafanyika chini ya uratibu wa Katibu wa Jimbo hilo, Juma Mwipopo, lengo ni kukileta chama karibu na wananchi.
Miongoni mwa matawi ya msingi yaliyozinduliwa hivi karibuni ni Tawi la Msingi la Mnarani, Mtaa wa Gurukakwalala na kufanyika pia uchaguzi wa viongozi wa tawi hilo uliosimamiwa na Katibu wa Jimbo, Mwipopo.
Viongozi waliochaguliwa kuongoza tawi hilo ni pamoja na Bwawa Moses (Mwenyekiti) na Esther Moses (Katibu). Mwakilishi wa Vijana alichaguliwa Salum Mayambe, mwakilishi wa kina mama ni Georgina Jackson na mwakilishi wa wazee ni Deogratius Joram. Vilevile alichaguliwa balozi wa nyumba kumi, Ipyana Noah.
Akitoa maelezo mafupi kabla ya uchaguzi wa viongozi hao, Mwipopo aliwataka wanachama na wapenzi wa CHADEMA kujitokeza hadharani ili chama kiwatambue kuwa wapo, wanakiunga mkono na wanakitumikia kwa uadilifu.
Aidha, Mwipopo alibainisha kuwa lengo la kufungua matawi ya msingi ni kuwatambua wanachama na kuwa na mtandao wa viongozi kuanzia ngazi ya chini na kuwahimiza viongozi waliochaguliwa kutimiza vema wajibu wao kwa kuwatumikia wananchi bila upendeleo.
Akizungumzia kuhusu kukithiri kwa rushwa katika jamii, Mwipopo aliwaonya waliohudhuria katika hafla hiyo kuwachagua viongozi kulingana na sifa zao na si kwa vigezo vya rushwa, urafiki na kufahamiana ili kujitofautisha na vyama vingine vya siasa.
No comments:
Post a Comment