Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amechafuliwa baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni mahasimu wake wa kisiasa kutengeneza picha chafu zinazomdhalilisha na familia yake na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii na simu za mikononi.
Akizungumza jana ofisini kwake, Lema alisema picha hizo zilitumwa Oktoba 29, mwaka huu kwenye simu ya mkononi ya mke wake, Neema.
Alisema kwa bahati mbaya, mtoto wake mwenye umri wa miaka saba, alipokea na kukutana nazo, hali ambayo ilimshtuka na kumwonyesha mama yake picha hizo.
Lema alisema baada ya kushuhudia ujinga huo, mke wake alimtumia Mchungaji Peter Msigwa kwenye simu yake ili amwonyeshe Lema siasa chafu zinazofanywa Arusha.
“Lakini mimi ninachosikitika sana ni picha hizi kupelekwa hadi kwa wakwe zangu na mama yangu mzazi, ambao wameniambia kama siasa inafikia hapa bora niache siasa,” alisema Lema.
Alisema baada ya kufikiria hatua za kufanya, alitoa nakala nyingi na kupeleka ofisi ya Bunge, ambako alimwonyesha Spika wa Bunge, Anne Makinda, na Naibu wake, Job Ndugai, ambao walisikitishwa kuziona picha hizo na kuahidi kumsaka mhusika ili ashughulikiwe.
Kwa mujibu wa Lema, kuna namba za simu za mkononi zinazotumiwa kumchafua pia, ambazo zinatuma meseji chafu kwa viongozi wa dini mbalimbali na watu wengine na kisha kuzimwa.
Alisema wahusika wakipiga namba hiyo simu zinaingia kwa Lema na kuanza kuulizwa juu ya ujumbe wake aliotuma.
“Yaani kwa siku naweza kupokea simu zaidi ya 200 za watu wakilalamika kuwatumia ujumbe wa matusi na kuniuliza kama nina akili timamu. Lakini mimi nasema Mungu atashughulika na hawa watu, japo tumejaribu kama chama kufuatilia Airtel wakatujibu tuachane na hilo jambo tutakufa,” alisema Lema.
Lema alisema alipeleka malalamiko katika Ofisi ya Bunge kwa njia ya barua yenye Kumbukumbu namba 011/11/2013 ikilalamikia picha chafu na namba hizo za simu.
Alitaja namba hizo za simu kuwa ni kuwa 0787717733, 0684941134, 0752593773 na 0688913046, ambazo zinatumiwa kumchafua. NIPASHE ilijaribu kupiga simu hizo zote jana mara kadhaa zote ama zilikuwa zimezimwa au hazipatikani.
Kuhusu kupeleka suala lake polisi, alisema hawezi kwa sababu ya suala hilo lipo mikononi mwa Ofisi ya Bunge, ambayo ni taasisi kubwa na inashughulikia kwa uzito wa kipekee.
“Lakini picha hizi nasambaza katika mikutano yangu yote, watu waone siasa chafu za Mkoa wa Arusha na wajue jinsi viongozi tunavyotoa maisha yetu,” alisema Lema kwa masikitiko.
Aliwaomba wafuasi wa chama chake kutolipiza kisasi kwa mtu yeyote, badala yake wamwachie Mungu na kuahidi kusambaza picha hizo kwa wafuasi wake ili waone propaganda chafu dhidi yake.
Naye Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema wamesikitishwa na mchezo mchafu unaofanywa na wapinzani wao wakubwa wa kisiasa na kuomba serikali kuwaonya vijana wanaotumiwa kutengeneza picha hizo ili wasiendelee.
Kwa upande wa mke wa Lema, Neema alisema alipoona picha hizo alishtuka na akiwa katika hali hiyo, alipigiwa simu na mama yake mzazi akilia na kumsihi amwombe mume wake aachane na siasa, sababu zimefikia mahali pabaya.
“Mimi nikamwambia mama usihofu na hapa Mungu anakwenda kutenda kitu. Hivyo, haya yote ni mapito tu yatapita,” alisema Neema.
No comments:
Post a Comment