CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mji wa Tunduma, wilayani Momba, mkoani Mbeya kimemtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Abiud Saidea, kumchukulia hatua za kinidhamu Mkurugenzi wa Halmashuri ya mji mdogo wa Tunduma, Aidan Mwanshinga na Mhasibu wake, Asu Kafabo, baada ya kutajwa kuwa ni watu walioshiriki kutoa zabuni kwa mawakala wa kukusanya ushuru katika vyanzo mbalimbali vya mapato kwa kampuni zisizo na sifa.
Wito huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Momba, Joseph China, katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kisimani, nje ya Soko la Manzese, ambao ulikuwa na lengo la kuwaeleza wananchi wa mji wa Tunduma sababu ya wajumbe wanane wa CHADEMA kususia kikao cha Baraza za Halmashauri kilichofanyika Novemba 8, mwaka huu.
Mwenyekiti huyo alisema chama chake kimeamua kufanya mkutano huo ili kutoa tamko la kumtaka Mkuu wa Wilaya na Mkoa, Abbas Kandoro, kuwachukulia hata za kinidhamu watumishi hao baada ya kutajwa na kamati ya muda kwamba wamekuwa wakitoa zabuni kwa watu wasio na sifa.
Alisema katika taairifa ya kamati hiyo ambayo iliwasilishwa mbele ya wajumbe wa baraza, inataja moja kwa moja kuwa wazabuni waliopewa kazi ya kukusanya mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya halmashauri walipewa kinyume cha sheria.
‘Ndugu zangu katika taarifa ya kamati watumishi hawa wanatajwa kuwa ndio walihusika kutoa tenda kwa watu wasio na sifa kwani baadhi yao walisema wazi kwamba walitoa fedha kwa watumishi hao ndiyo maana wakapata tenda hiyo,” alisema China.
China alisema watu waliohojiwa na kamati hiyo walisema pamoja na zabuni hiyo kutangazwa, ilikuwa ni geresha tu kwani mkurugenzi na mhasibu wake walishapanga watu wao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Frank Mwakajoka, alisema katika vyanzo ambavyo tenda hizo zimetolewa kwa watu wasio na sifa ni pamoja na kukusanya ushuru wa mazao, ushuru wa machinjio, ushuru wa maliasili, ushuru wa maegesho ya magari na ushuru wa magari yanayovuka mpaka huo.
Alisema kutokana na hali hiyo wanautaka uongozi wa wilaya pamoja na mkoa kuwaondoa watumishi hao katika mji huo, vinginevyo chama hicho kitaitisha maandamano kwa lengo la kuwaondoa watumishi hao.
No comments:
Post a Comment