Sunday, November 17, 2013

CCM yachezeshwa shere Shinyanga

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Adam Ngalawa, juzi alipatwa na fedheha kubwa baada ya Katibu Mwenezi wa CHADEMA, Tawi la Bulyanhulu, Kata ya Kakola, Philemon James, kukataa hadharani mpango wa kununuliwa ili ajiunge na chama hicho.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bulyanhulu, Emmanuel Gombega, alisema mkakati wa viongozi wa CCM katika eneo hilo kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa, kuwashawishi wanachama wa CHADEMA kwa fedha ulianza muda mrefu katika eneo hilo.
Alisema kuwa wiki moja iliyopita walifanikiwa kumshawishi James na mwanachama mwingine wa CHADEMA kwa kuwapatia kiasi cha sh 300,000 kwa lengo la kuangamiza nguvu za chama hicho cha upinzani katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Gombega, baada ya viongozi hao kukubaliana na James, waliandaa mkutano wa hadhara na kumualika Katibu wa CCM mkoa kwa ajili ya kumpokea mwanachama huyo wa CHADEMA mwenye na nguvu za ushawishi kwa wananchi wa Bulyanhulu.
“Kila hatua waliyokuwa wakifanya, James alikuwa anafikisha taarifa kwa uongozi wa CHADEMA, tukamueleza sasa ni wakati wa kula fedha zao na kuwakataa hadharani,” alisema Gombeza.
Aliongeza kuwa kabla ya mkutano uliohutubiwa na Ngalawa, walifanya kazi ya kuwashawishi wananchi wahudhurie kwa wingi wakijua kitakachotokea.
Baada ya katibu huyo wa mkoa kumaliza kuhutubia, mshereheshaji katika mkutano huo alimuita James jukwaani kwa lengo la kurudisha kadi ya CHADEMA na kukabidhiwa ya CCM.
James alipanda jukwani na wafuasi na viongozi wa CCM kumvisha shati pamoja na khanga za chama chao.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa CHADEMA, baada ya James kuvishwa vitu hivyo, aliwaomba viongozi walio jukwaani wampatie kipaza sauti na watulie kumsikiliza.
Ndipo akawaeleza kuwa suala la kuwa katika chama chochote ni hiyari ya mtu na siyo ushawishi wa fedha.
“Baada ya kuwaeleza hivyo, akavua zile sare na kuwaambia hawezi kuondoka CHADEMA na kusaliti mageuzi, hali iliyomfanya Mwenyekiti wa CCM wa tawi aanguke chini kwa kuchanganyikiwa huku katibu wa mkoa, akilaumu kwa namna viongozi wake walivyoandaa mkutano wa kumfedhehesha,” alisema.
Tanzania Daima iliwasiliana na Ngalawa kuthibitisha tukio hilo la chama chake kuwanunua wapinzani, ambapo alikiri kufanya mkutano wa hadhara katika eneo.
Pia alikiri James kupanda jukwaani huku akikanusha kuwapo kwa mkakati wa kuwanunua wanachama wa vyama vingine wajiunge na CCM.
“Ni kweli nilikuwa Kakola na mmoja wa wananchi aliomba kipaza sauti akauliza maswali, lakini hakuna mtu aliyeshawishi kuwanunua wanachama wa vyama vingine, na hata huyo unayemsema hana hadhi ya kununuliwa,” alisema Ngalawa.
Alipoulizwa sifa za wanachama wa vyama vingine wanaopaswa kununuliwa, Ngalawa alisema CCM hakina utaratibu wa kuwanunua wananchi.

1 comment: