Sunday, November 17, 2013

Sitta afyatua bomu

Awapa `vidonge` mahasimu wanaofukuzia urais
Atoboa walivyoandaa bajeti bil.10/- za rushwa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amefyatuka na kuwananga mahasimu wake wanaowania urais wa 2015 kwa kuandaa bajeti ya zaidi ya Sh. bilioni 10 ili waingie madarakani kwa njia ya rushwa.
Amedai kuwa watu hao wamekula yamini ya nchi kuongozwa na mtu tajiri kupitia njia ya mkato.
Aidha, akasema kuna hatari wakati taifa likielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani, na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kuzuka kwa kundi la matajiri, ambao wengi wao ni wakwepa kodi mashuhuri, watoroshaji wa madini ya nchi na watoroshaji wa nyara na maliasili za nchi.
Akizungumza jana katika mahafali ya 17 ya Shule ya Sekondari ndogo ya Agape inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Sitta alisema walafi hao wa madaraka ni pamoja na baadhi ya viongozi waliojitajirisha kupitia fursa za serikali kwa njia ya rushwa, mikataba mibovu, wauza madawa ya kulevya na mawakala wa maovu.
Alisema kutokana na mwelekeo huo potofu, amewataka wananchi wamruhusu kutumia hadhara hiyo kuzungumzia hatari kubwa inayoikabili nchi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Katika mazingira haya inasikitisha kwamba viongozi wengi hususani wenye uroho wa madaraka na mali wamejigeuza kuwa wachekeshaji wa mfalme kwa kumuunga mkono, kujipendekeza na kumsifia kiongozi wanayejua maovu yake kwa mategemeo ya kupewa fedha na vyeo. Watu hao katika miaka miwili wamejipambanua kwa njia ya harambee mbalimbali zinazotangazwa kwa mbwembwe na kelele katika baadhi ya makanisa, misikiti na makundi mengine ya jamii,” alisisitiza.
Alisema kuwa hadi sasa, watu hao wamechangia fedha zinazokadiriwa kufikia Shilingi bilioni saba huku wakiwa wameshaandaa bajeti ya bilioni 10 kwa ajili ya rushwa ya uchaguzi ambayo hawataki iitwe rushwa kwa sababu macho yao yamepofuka.
Alisema kuwa Watanzania hawahitaji shahada ya siasa kubaini watu hao wakifanikiwa katika malengo yao. Alisema uongozi utakaotokana na genge hilo hautaweza kuleta neema kwa Tanzania kwa kuwa ngazi zote za uongozi katika himaya ya aina hiyo, zitajazwa na watu wanaofanana katika maadili potofu.
“Masikini na wanyonge watabanwa mbavu zaidi, matabaka ya wenye utajiri na masikini yatapanuka kiwango ambacho hakitavumilika. Lakini pia ukusanyaji wa kodi na mapato mengine ya serikali utadorora na kudidimiza huduma zote za jamii na kipato cha kila Mtanzania… hatimaye misingi yetu ya umoja na usawa itabomoka na kulitumbukiza taifa katika machafuko,” alisema.
Kuhusu hatma ya taifa kabla na baada ya uchaguzi mkuu, Sitta alisema Watanzania wasipokuwa na mtazamo wa kizalendo na wakasimama kwa dhati ya mioyo yao kupambana na kulikataa jambo hilo, watawaachia watoto wao urithi ambao utatafuna vizazi hata vizazi.
“Dhambi kubwa katika taifa lolote ni pale mbele ya maovu, watu wema wanaamua kukaa kimya. Mimi na wewe tukiamua hali hii ikome sasa, inawezekana na cha msingi ni kurudi nyuma na kujipanga upya kupambana na hali hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Kuhusu suala la maamuzi magumu, Sitta alisema tatizo jingine linalodhihirisha mgawanyiko wa kitabaka ni kiburi cha baadhi ya viongozi ambao wanatamba kwamba hawawajibiki kwa vyombo vya sheria kama wafanyavyo watu wa kawaida.
Sitta ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo yaliyoambatana na harambee ya kuchangia ujenzi wa chepo ya Seminari hiyo, alichangia Sh. 5,750,000.
Awali akisoma risala ya wahitimu wa seminari hiyo, Shaine Mapunda, alisema inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa zahanati ya shule ambayo husababisha wanafunzi kukosa masomo kwa ajili ya kufuata matibabu hospitali ya Marangu.
“Tunaomba kuongezewa vitabu vya michepuo ya sanaa ili kuongeza ufaulu na ubora kwa wanafunzi wa michepuo ya sanaa, uboreshaji wa viwanja vya michezo ufanyike kwa awamu ili kuzidi kukuza na kuinua vipaji vya michezo mbalimbali,” alisema Shaine.
Mkuu wa Shule hiyo, Sista Elistaha Mlay, alisema shule hiyo yenye mikondo ya kidato cha tano na cha sita yenye jumla ya wanafunzi 548, inakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji na umeme hali inayosababisha kero kwa wanafunzi kujisomea. Jumla ya wanafunzi 108 wa kidato cha nne wamehitimu.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment