Monday, October 7, 2013

Zitto: Tunataka Katiba Mpya iwajali Wakulima na Wananchi wa Vijijini

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa Mh. Zitto Kabwe (Mb) amesema Katiba Mpya ni lazima iwajali Wakulima na Wananchi wanaoishi vijijini hapa nchini maana wametelekezwa kwa muda mrefu, kudhulumiwa na kufanywa maskini wa kutupwa.
Zitto amesema Wananchi wengi wa vijijini hasa wa Kanda ya Magharibi wanapata shida leo kwa kichagua CCM ambapo Wabunge wao wamekuwa hawawatetei Bungeni wala hawaulizi maswali na wengine kutetea maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya Wananchi hao.
Amesema Waziri Mkuu Mizengo Pinda tangu achaguliwe hajawahi kuuliza swali Bungeni kwa sababu alipochaguliwa tu aliteuliwa kuwa Waziri matokeo yake Wananchi wa Jimbo lake wanakosa mtu wa kuwawasilishia hoja zao Bungeni. “Pinda hata ukimwambia aandike swali kwa taratibu za kibunge hajui ni kama walivyokuwa wenzie akina Abdallah Kigoda na Mark Mwandosya ambao tangu walipochaguliwa tu waliteuliwa kuwa Mawaziri, hawawezi hata kuandika maswali. Kigoda alipata shida kweli kuuliza maswali alipoachwa kwenye Baraza la kwanza la Mawaziri la Rais Kikwete” Alisema Zitto.
Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mwajalila katika Kata ya Mpanda ndogo Zitto alimshangaa Mbunge wa Jimbo la Mpanda Magharibi Moshi Selemani Kakoso ambaye badala ya kutetea Wananchi wake wapate bei nzuri ya Tumbaku, Mbolea kwa wakati na watibiwe kwa mfuko wa Bima ya afya ambao wamekuwa wakiuchangia Tsh 10,000/= kwa mwaka bila kupata dawa wala huduma yoyote wanapoumwa; Mbunge huyo kazi yake ni kuzunguka Dar es salaam na kufanya mikutano na waandishi wa habari kunusuru ulaji wake wa APEX uliofutwa na Bunge kwenye vyamavya ushirika. (Kakoso alikuwa ni Mwenyekiti wa Shirika la APEX ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likiwalangua wakulima wa Tumbaku nchini kwa muda mrefu kabla halijafutwa na sheria ya Bunge). 
Akiwa katika Kijiji cha Karema kilichokuwa Makao Makuu ya Jimbo la Magharibi enzi za Mkoloni na kilichogunduliwa na Wamisionari wa Kigiriki toka Kongo Zitto aliwaambia Wananchi wa eneo hilo “Si mnaona hata mradi wenu wa Bandari hapa Kijiji na Tarafa ya Karema mmepewa Mkandarasi feki wakati sisi kule Kigoma Bandari karibia inakamilika ni kwasababu wanajua Kigoma yuko Zitto na hapa yuko mbunge dhaifu na mwizi mwenzao wa CCM” alisema Zitto
Tunataka Katiba Mpya izuie Wabunge kuwa Mawaziri na iwape nguvu Wananchi ya kuwawajibisha Wabunge ambao hawawasilishi maslahi yao kwa kuwaondoa madarakani na kuchagua wengine.
Akizungumzia Pensheni kwa Wakulima Zitto amesema Taifa hili linaendeshwa na Wakulima ambao wanachangia sehemu kubwa sana ya pato la taifa, lakini wanapochoka kwa maradhi au uzee wanaishia kuwa ombaomba na mzigo kwa familia zao kwa kukosa pensheni ya uzeeni hali ya kuwa nguvu yao iliishia katika kulijenga Taifa. “Si haki mfanyakazi wa ofisini apate NSSF na pensheni za uzeeni wakati mkulima anayemlisha na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa akizeeka ndio mwisho wake wa kujitegemea” alisema Zitto.
Ziara ya Zitto leo ilifanyika katika Jimbo la Mpanda Magharibi ambapo amezindua vijiwe 20 vya Chama, kupokea kadi 150 za waliokuwa Wanachama wa CCM katika vijiji vya Mwajalila, Kasekese,Kapalamsenga, Karema (Bismarkburg enzi za Mjerumani) na Ikola, akiwemo Kampeni Meneja wa Mbunge Kakoso wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010. Ziara itaendelea ya Mh.Zitto kesho katika Jimbo la Mpanda Mjini ambapo jioni kutafanyika Mkutano Mkubwa sana wa hadhara. Ziara hii ni utekelezaji wa Program ya CHADEMA NI MSINGI


Chanzo : Kurugenzi ya Habari Chadema

No comments:

Post a Comment