Thursday, October 17, 2013

Zitto awavuruga viongozi

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema anawashangaa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumuweka kitimoto baada ya kuanika viwango vya mishahara ya viongozi.
Hivi karibuni akiwa kwenye ziara ya kuimarisha chama chake Kanda ya Magharibi, Zitto alitaja viwango vya mishahara wanayolipwa wabunge, mawaziri, waziri mkuu na rais.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Zitto alisema kuwa aliwashangaa wabunge wa CCM kumuweka kitimoto kuhusu jambo hilo wakiwa kwenye kamati za Bunge.
“Niliwaambia kwamba mbona hata mshahara wa Rais wa Marekani, Barack Obama, umewekwa mitandaoni ukionesha analipwa dola 400,000?” alihoji.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alihoji ni kwanini viongozi wa hapa nchini hawapendi kuwaeleza wananchi mishahara wanayopata, ukiwamo wa rais anayelipwa sh milioni 384 kwa mwaka.
“Nilipoingia Ofisi Ndogo za Bunge juzi, baadhi ya wabunge walianza kunishambulia kwa maneno wakitaka kujua sababu za kutaja mshahara wa rais.
“Niliwauliza kwani kuna tatizo gani kuutaja wakati amechaguliwa na wananchi na hiyo fedha anayolipwa ni kodi yao? Nikawahoji, pale Ikulu kuna kazi ngumu anayofanya?” alisema.
Zitto aliongeza kuwa rais anasafiri, anavalishwa, anakula bure kwa fedha za wananchi, sasa kwa nini mshahara wake wasiujue, na kwa nini usikatwe kodi.
Aliongeza kuwa sababu ya kutaja mishahara ya viongozi wa juu wa serikali ni kuwaeleza wananchi wajue ukweli ndipo wapate hasira pindi wanapocheleweshewa maendeleo katika maeneo yao.
Zitto aliongeza kuwa wabunge wanalipwa mshahara wa sh milioni 11.2 kwa mwezi kwa kazi ya kuzungumza pekee, huku posho ikiwa ni sh 330,000 kila siku.
“Mambo kama hayo ni lazima wananchi wayajue na ndiyo maana wabunge hawataki yajulikane, kwa sababu wananchi wakiyafahamu watawabana wawajibike katika nafasi zao,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya Katiba mpya, Zitto aliwalaumu wabunge wa CCM kwa kutokuwa na nia ya kupatikana kwa katiba hiyo kutokana na mizengwe waliyomfanyia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wakishirikiana na Naibu Spika, Job Ndugai.
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Chang’ombe, Edith Bunjoro, maarufu kama Mama Kevin, aliwataka wananchi wa kata hiyo kumuunga mkono katika juhudi zake za kulikomboa jimbo hilo kutoka mikononi mwa CCM.

No comments:

Post a Comment