MBUNGE wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (CHADEMA), amesema kwamba amefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji na barabara jimboni humo.
Wenje ambaye pia ni Waziri Kivuli katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Msingi Buhongwa jijini Mwanza.
Alisema kwamba, hadi sasa amefanikiwa kugawa madawati kwa karibu shule zote 81 za jimbo lake hilo la Nyamagana, hivyo kupunguza sana tatizo la wanafunzi kukaa chini, tofauti na ilivyokuwa kwenye uongozi wa CCM miaka kadhaa iliyopita.
Alisema kutokana na harakati zake za kupigania maendeleo ya wananchi wa Nyamagana, amefanikiwa pia kukabidhi maabara ya kisasa inayotembea, ambayo itafanya kazi kwa shule zote 30 za sekondari Nyamagana.
Katika mkutano huo, Wenje aliitaja miradi mingine ya kimaendeleo iliyotekelezwa na inayotekelezwa kwa sasa chini ya uongozi wake kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami ya Stesheni-Karuta, Mkuyuni-Butimba, Isamilo na kadhalika, ambazo tayari ujenzi wake ulishakamilika.
“Kwa muda wote tangu mnichague mwaka 2010, nimekuwa na harakati za kusimamia na kuchochea utekelezwaji wa miradi ya maendeleo. Na hata ninyi ni mashahidi, maana hata barabara ya Pepsi-Igogo tunaijenga kwa lami,” alisema Wenje.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa Nyamagana, miradi mingine iliyopo kwenye utekelezwaji sasa na gharama zake kwenye mabano ni ujenzi wa wodi ya wazazi Mahina (sh milioni 20) na ujenzi wa zahanati ya Isamilo (sh milioni 15).
Mingine ni ujenzi wa zahanati ya Isebanda Buhongwa (sh milioni 15), kuezeka Shule ya Mkuyuni (sh milioni 8.5), kununua maabara ya kisasa inayotembea kwa ajili ya shule za sekondari katika Jimbo lake la Nyamagana, iliyogharimu sh milioni 5.9, na fedha zote hizo zinatokana na mfuko wa jimbo.
Aidha, Wenje aliwaeleza wananchi hao kwamba, kwa sasa pia kuna ujenzi wa zahanati nyingine huko Bulale - Buhongwa yenye thamani ya sh milioni 60, pamoja na zahanati nyingine ya Mkuyuni, inayojengwa kwa gharama ya sh milioni 60, ambapo tangu tupate uhuru Mkuyuni haijawahi kuwa na zahanati.
Aliwaahidi pia kushughulikia upatikanaji wa umeme kwa wananchi wanaoishi maeneo ya Kishili, Kata ya Igoma, ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya kata zote 13 za Nyamagana.
No comments:
Post a Comment