Vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi vimesema vitaweka hadharani kesho mambo yaliyojiri katika mazungumzo yao na Rais Jakaya Kikwete yaliyofanyika Ikulu, Jumanne wiki hii.
Viongozi wakuu wa vyama hivyo juzi walikutana na Rais Kikwete kuzungumzia kasoro wanazolalamikia kuwamo kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013.
“Tumepanga kuzungumza na waandishi wa habari Ijumaa (kesho) kuelezea mambo yaliyojiri katika mazungumzo yetu na Rais Kikwete,” alisema Naibu Katibu Mkuu CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema ushirikiano wa vyama wamekubaliana kuzungumza baada ya kukutana na kutafakari yote yaliyojiri kwenye mazungumzo kwa upana na kuandaa mapendekezo yanayohitajika.
Rais Kikwete juzi alikutana na viongozi wa vyama sita vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Baadaye, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema pande mbili hizo zilikubaliana katika mazungumzo hayo mambo makuu mawili.
La kwanza, vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha muswada huo, kuyawasilisha haraka serikalini ili kutafuta namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
La pili, vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi kwa maslahi mapana ya nchi na mustakabali wa taifa.
Taarifa hiyo ilieleza katika makubaliano hayo, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi ulimalizika kwa pande mbili hizo kukubaliana mambo hayo.
Viongozi, ambao Rais Kikwete alikutana nao juzi kwa mazungumzo hayo wanatoka vyama vya CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP.
No comments:
Post a Comment