Thursday, October 17, 2013

CHADEMA kusomesha wanafunzi bure

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Manispaa ya Morogoro kinakusudia kudondosha neema ya elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari mjini humo ili kuwapunguzia mzigo wa ukali wa maisha wazazi.
Hayo yamebainishwa kwenye mkutano wa kuimarisha chama uliofanyika Kwamgulasi, Kata ya Chamwino na kuhutubiwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwamo Mwenyekiti wa Vijana wa chama hicho wa mkoa (BAVICHA), Ngonyani Ngonyani, Katibu Mwenezi wa Manispaa, Elias Mwalusako na Mwenyekiti wa chama wa kata hiyo, James John.
Kwa wakati tofauti walisema uwezo wa manispaa kutumia fedha zake za ndani kufuta ada na michango mashuleni ni mkubwa na kuwa kinachoifanya ishindwe kufanya hivyo ni wizi wa fedha za umma.
“Kwa makusanyo ya adhabu ndogodogo ambazo manispaa imejiwekea zikiwamo shilingi 50,000 kwa anayekamatwa akichafua mazingira, wanafunzi wanaweza kusoma bure na huduma za afya kuboreka, watu tukapata tiba sahihi na bure,” alisema James.
Kwa wakati tofauti wakitoa matatizo yaliyomo kwenye halmashauri hiyo, likiwamo la kushindwa katika makusanyo na Halmashauri ya Kilombero iliyofikia zaidi ya shilingi bil. 1, walisema fedha nyingi za umma ambazo zilikuwa zifute michango na ada mashuleni katika manispaa hiyo zinavuja mikononi mwa viongozi na kuwabebesha zigo la kodi, ushuru na michango wananchi wasio na hatia.
“Lazima fedha zinazoundiwa sheria na kukusanywa kwa umma zielekezwe kwenye shughuli muhimu, mfano makusanyo ya uchafuzi wa mazingira, kwanza zitolewe taarifa mapema kwa wananchi na ziende kwenye elimu na afya…leo hii hatujui tangu waanze kukusanya wamepata kiasi gani na zimefanya nini,” alisema Ngonyani.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi, Mwalusako, aliwaomba wananchi kuwaunga mkono wanasiasa na waandishi wa habari nchini katika shughuli zao kutokana na matukio yanayowakuta katika kazi zao.

No comments:

Post a Comment