Monday, September 9, 2013

Kilombero walilia Tanganyika Katiba mpya

BARAZA la Katiba lililoandaliwa na asasi zisizo za kiserikali mkoani Morogoro za Volunteer Group na Kijogoo Group, limeitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuondoa neno Tanzania Bara katika rasimu iliyopo na kurejesha Tanganyika ili kukamilisha Muungano.
Baraza hilo lilitoa pendekezo hilo hivi katika mkutano uliofadhiliwa na Foundation For Civil Society mjini hapa.
Pendekezo hilo lilikwenda sambamba na kuunga mkono muundo wa serikali tatu kwenye rasimu hiyo na kutaka kuongezwa neno ‘usawa’ kwenye mambo ya Muungano kama dira ya mshikamano baina ya Zanzibar na Tanganyika.
Baadhi ya washiriki wa baraza hilo lililokuwa na washiriki zaidi ya 200; Ramadhan Chakachale na Upendo Rajabu kwa nyakati tofauti walisema kimsingi rasimu imeandaliwa vizuri licha ya marekebisho madogo kama yanavyojitokeza.
“Kimsingi sisi tumechelewa sana, ilitakiwa serikali yetu ya Tanganyika tuidai tangu mwaka 1964, kwani wenzetu licha ya kuungana bado waliendelea kuwa na serikali,” alisema Upendo.
Aidha, kutokana na kuanza kushamiri kwa dawa za kulevya, Katiba itamke kuwanyonga watakaobainika sambamba na watakaokumbwa na makosa ya mauaji na ufisadi.
Waratibu wa baraza hilo akiwamo Mwenyekiti wa Volunteer Group, Avelyni Ligohalimu na Ramadhan Said wa Kijogoo Group, walitaka washiriki kutafakari kwa kina marekebisho katika rasimu hiyo na kuchangia kwa kina, ili mawazo yao yapenye na kuingia kwenye Katiba.

No comments:

Post a Comment