Monday, September 9, 2013

Wabunge CHADEMA kuanza ziara

WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Ziwa Mashariki, wanatarajiwa kuanza ziara katika mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga, kwa ajili ya kuimarisha chama na kuwaeleza wananchi sababu za kutokea vurugu bungeni.
Akizungumza juzi na Tanzania Daima, mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, alisema kuwa ziara hiyo itakuwa na ajenda nne muhimu.
Alizitaja ajenda za ziara ya operesheni hiyo kuwa ni kuwaeleza wananchi sababu ya vurugu zilizotokea hivi karibuni bungeni, mambo ya Katiba mpya, kujenga na kuimarisha chama na kuzungumzia kilimo cha pamba.
Alisema katika ziara hiyo itakayoanzia Musoma mkoani mkoani Mara na baadaye kwenye majimbo mengine ya mikoa hiyo, pia watazungumzia hali ya maendeleo, umaskini na changamoto zilizopo tangu uhuru mwaka 1961.
"Tunakwenda kuwaambia wananchi kuhusu kilimo cha pamba na changamoto zake, kujenga na kuimarisha chama chetu. Kwa hiyo naomba sana wajitokeze kwa wingi watuunge mkono katika harakati zetu," alisema Nyerere.
Alisema kuwa wabunge wengine watakaokuwa kwenye oparesheni hiyo ni Meshack Opulukwa (Meatu), Silvester Kasulumbayi (Maswa Mashariki), Ester Matiku (Viti Maalum Mara) na John Shibuda (Maswa Magharibi).
Nyerere alisema kivumbi cha ziara hiyo kitaanza hivi karibuni mara baada ya taratibu za kichama kukamilika na kuwaomba wanachama wote wa CHADEMA wenye nia ya kugombea nafasi yoyote kupitia chama hicho nao kujitokeze kwa wingi.

No comments:

Post a Comment