Thursday, August 8, 2013

Warioba avishtukia vyama

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema kuwa wamebaini ujanja unaofanywa na vyama vya siasa nchini wa kutoa miongozo inayolenga kuwaeleza wananchi maoni ya kutoa katika mikutano ya mabaraza ya Katiba.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa Baraza la Katiba la Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania, waliokuwa wakijadili rasimu ya Katiba mjini Bagamoyo, mkoani Pwani jana, Jaji Warioba alivitaka vyama viache tabia hiyo.
Alisema tume imegundua ujanja wa vyama hivyo na kwamba maoni yaliyomo katika rasimu hiyo yametolewa na kundi kubwa la Watanzania wenye akili timamu, kwa hiyo mawazo yao lazima yaheshimiwe.
Jaji Warioba alisema wananchi waachwe watoe maoni yao katika mabaraza ya Katiba kwa kuwa jamii imewachagua kutoa maoni yaliyojadiliwa kupitia kata zao.
Aliongeza kuwa wajumbe wa mabaraza hayo watapitia kila sura ya rasimu hiyo ili kupata mawazo halisi huku ikionesha sura nyingine ya rasimu hiyo ambayo wananchi walitoa maoni ambayo hayatokani na mawazo yao.
Jaji Warioba alisisitiza kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa sasa na vyama ni sawa na kutafuta mchawi, kwa kuwa tume imepokea maoni yanayotokana na mawazo ya Watanzania wenye akili timamu.
“Unaweza kutofautiana nao lakini lazima uheshimu mawazo yao ambayo hayakuwa na itikadi ya vyama vya siasa,” alisema.
Aidha, Jaji Warioba aliwataka wanasiasa kuacha kulumbana kwa kuwa wanapoteza muda na kuwataka kujielekeza katika kuijadili rasimu hiyo.
“Hivi sasa kampeni zinafanyika katika majukwaa na tume haitachukua maoni ya vyama vya siasa yanayotolewa majukwaani, tutayapokea maoni yanayotolewa kwa utaratibu uliopangwa,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge Wanawake, Anna Abdallah, alisema moja ya mambo waliyoyapendekeza ni kutaka kutokuwapo kwa ukomo wa mbunge kugombea jimbo.
Alisema pia wamejadili haki za wanawake, hasa katika kurithi mali na kumilikishwa ardhi na kupendekeza Katiba imtamke mwanamke na ushiriki wake katika masuala mbalimbali.

No comments:

Post a Comment