Thursday, August 8, 2013

Diwani aweka taa za barabarani

DIWANI wa Longuo B, Raymond Mboya (CHADEMA), amejitolea kuweka taa kwenye barabara za Mtaa wa Kitandu ambao upo karibu na Hospitali ya Rufaa ya KCMC baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kufanyiwa vitendo vya ubakaji na wizi.
Diwani Mboya alisema jana kuwa alipokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa udaktari wanaosoma KCMC kwenye mkutano alioufanya Juni mwaka huu juu ya kuwapo kwa changamoto ya matukio hayo.
Alisema licha kuweka ulinzi jamii, lakini ilionesha kutozaa matunda hivyo kuamua kuweka nguzo pamoja na taa kwenye barabara ya mtaa huo.
Mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Kitandu akizungumza na Tanzania Daima, Alex Mbaga alisema vitendo vya wizi vilikuwa vimekithiri kutokana na barabara hizo kutokuwa na taa za barabarani na kuwa na giza, hivyo majambazi kutumia nafasi hiyo kuwaibia watu.
Alisema kwananchi waliokuwa wahanga wa matukio hayo ni wanafunzi wanaosoma udaktari kwenye Chuo cha KCMC, wale wa Ushirika (MucoBs) pamoja na Mwenge ambao wamepanga nje ya vyuo kwenye mtaa huo.
Mwananchi mwingine, Jeofrey Moras, alisema umefika wakati wananchi wa eneo hilo kulala bila kufunga mageti yao ili ikitokea wanafunzi hao wanapokimbizwa na majambazi kuweza kukimbia kwenye nyumba hizo ili kujiokoa.

No comments:

Post a Comment