Baadhi ya wanasheria, wasomi na wanasiasa wameishambulia serikali na Polisi kwa kutengeneza kesi na kuwabambikia watu na kuwapeleka mahakamani ili kuzima mjadala pindi tukio la kihalifu linapotokea.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema tatizo la watu mbalimbali kufikishwa mahakamani na kisha kufutiwa mashtaka linatokana na Jeshi la Polisi nchini, kuchagua nani wa kumshtaki badala ya kumshtaki mtu aliyetenda kosa na kwamba wanafanya hivyo kutokana na kuwafurahisha wakubwa wao.
Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia, aliyasema hayo jana alipoulizwa na NIPASHE kuhusu wananchi kufutiwa mashtaka wanapofikishwa mahakamani.
Sungusia alisema Polisi wameshindwa kufanya kazi yao vilivyo na kuwashtaki watu waliotenda makosa badala yake wamekuwa wakichagua nani wamshtaki na wamshtaki kwa kosa gani wanalochagua wenyewe na kwamba ndiyo maana wakifikishwa mahakamani wanaonekana hawana hatia na kuachiwa huru.
Alisema pia ni kukosekana kwa mfumo mzuri wa utambuzi wa nani kafanya kosa na kafanya kosa la aina gani.
Alisema mapungufu hayo yanachangia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuandaa mashtaka dhaifu na matokeo yake watu wanapofikishwa mahakamani wanaonekana hawana kesi ya kujibu.
Sungusia alisema tatizo la Jeshi la Polisi nchini, ni kufanya kazi kwa maagizo ya kisiasa na kutaka kuwafurahisha wakubwa wao ili waonekana wanafanya kazi na kwamba kwa kuwa mahakama haishinikizwi, ndiyo maana wanapata aibu wanapombambikizia mtu kesi.
Kuhusu udhaifu wa sheria, Sungusia alisema mpaka sasa hakuna maana ya neno gaidi na kitu gani anachotenda mtu ahesabike kama ametenda kosa la ugaidi na ndiyo maana wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliowahi kuhusishwa na vitendo vya ugadi walifutiwa kesi.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla, alisema kuna tatizo la kubambikia watu kesi na kwamba hata mwaka uliopita alitoa maoni yake kwenye Siku ya Sheria kuwa mahabusu nyingi pamoja na magereza zimejaa watuhumiwa wa makosa ya kubambikiziwa.
Stolla alisema waendesha mashtaka wengi wanafanyakazi kibabe bila kuzingatia weledi ikiwa ni pamoja na kutokuelewa ni hatua na vigezo vipi vinavyofanya mtu ashtakiwe.
Stolla alihoji ni kwa nini mtu anakamatwa na kupelekwa mahakamani bila kuchuja vigezo vinavyotakiwa na kudai upelelezi bado haujakamilika na kuongeza kuwa huo ni uzembe wa hali ya juu wa kitaaluma na uendeshaji mashtaka.
“Kuna watu wanaelewa kabisa kuwa mtu huyu hashtakiki lakini kwa sababu za shinikizo na kubambikiza kuliko weledi, na mfano mzuri ni ule wa Tabora na ile kesi ya yule anayedaiwa kumteka na kumjeruhi Dk. Ulimboka katika akili ya kawaida mtu hawezi kukiri jambo kama lile,” alisema Stolla.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema ni vyema waliopewa kazi ya kupeleleza likafanyiwa tathmini kwani Ofisi ya DPP, inaonekana kuwa haijiandai vya kutosha, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na vigezo vinavyotakiwa.
Dk. Bana alifafanua kuwa, Ofisi hiyo inatakiwa kujitathmini upya kimkakati, kimaadili na kiweledi kwani kesi yoyote inapotakiwa kupelekwa mahakamni isiwe na shaka yoyote ili haki itendeke kuliko ilivyo sasa nyingi zinazopelekwa mahakamani ni za kutia shaka.
Mwanasheria wa kujitegemea, Frank Mwalongo, alisema haiwezekani kwa mtu mwenye akili timamu akakubali kujiingiza kwenye kosa la jinai ambalo hakuhusika huku akijua ni hatari.
Kwa mujibu wa Mwalongo, mchakato wa kesi hiyo ya Mkenya aliyedaiwa kumteka Dk. Ulimboka, ulitawaliwa na utata mwingi ikiwa ni pamoja na hukumu yenyewe juzi na kufunguliwa kwa shtaka jipya la uongo aliyodai imefunguliwa kwa ajili ya kuwaondolea maswali wananchi kwa manufaa ya umma.
CHADEMA, CUF WANENA
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema uamuzi wa DPP kuwasilisha mahakamani hati ya kutoendelea na mashtaka ni ishara ya wazi kwamba aliona mashtaka hayo hayakuwa na msingi na yalifunguliwa ili kutumia kisingizio cha kesi kuwa mahakamani, kudhibiti vyombo vya habari kuandika habari za uchunguzi akitolea mfano suala la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Steven Ulimboka.
Aidha, alisema mashitaka hayo yalifunguliwa pia kwa lengo la kulidhibiti Bunge lisijadili suala hilo na kuisimamia serikali ndiyo maana wengine walizuiwa kuhoji bungeni, kwa kisingizio kuwa suala liko mahakamani.
Mnyika alisema uamuzi wa mahakama uliotolewa juzi, unafungua mlango kwa vyombo vya habari kuandika habari za uchunguzi na wabunge kuhoji ukweli wa tukio hilo ambapo, watuhumiwa ni pamoja na anayedaiwa kuwa mtumishi wa Usalama wa Taifa.
“Kufuatia uamuzi wa DPP na Mahakama; Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkuu wa Jeshi hilo (IGP) Said Mwema na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova, ni muhimu wajitokeze kukiri kwamba, walilidanganya taifa kwa mwaka mmoja na waeleze ukweli wa nani hasa ni mtekaji na mtesaji wa Dk. Ulimboka kwa kutoa ripoti ya timu ya Msangi,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema kitendo cha wananchi ambao serikali imewashtaki kuachiwa na mahakama bila kuwa na kesi ya kujibu ni cha aibu na kinaonyesha namna serikali ilivyoshindwa kutimiza wajibu wake wa kulinda raia na haki zao.
“Serikali ina wajibu wa kulinda raia na haki zao, lakini badala ya kufanya hivyo, yenyewe imekuwa ikikimbilia kubambikia wananchi wake kesi na tena kesi zenyewe za jinai na si za madai,” alisema.
Mtatiro alisema kitendo hicho kinadhihirisha kwamba karibu nusu ya kesi zote za jinai walizoshtakiwa wananchi katika mahakama mbalimbali ni za kubambikiwa.
Alisema wana ushahidi kuwa kinachoendelea dhidi ya vyama vya siasa vya upinzani, ikiwa ni pamoja na kubambikia wanachama wa vyama hivyo kesi kunatokana na maelekezo ya serikali kwa watendaji wa serikali, ikiwa ni pamoja na polisi ya kuhakikisha wanawadhibiti wapinzani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema tatizo ni mfumo mbovu wa elimu akitolea mfano kuwa kuna kesi zimefikisha miaka 12 bila kutolewa hukumu huku wahusika wakiendelea kusota rumande.
No comments:
Post a Comment