Thursday, August 8, 2013

Warioba ashangaa mjadala wa Katiba kujikita maeneo machache

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema haridhishwi na namna wanasiasa na vyombo vya habari wanavyojadili Rasimu ya Katiba, kwa kujikita katika mambo yanayohusu utawala na madaraka pekee, huku wakiacha kujadili maeneo mengi yanayogusa wananchi.

Pia ameionya kampeni zinazodaiwa kufanywa na baadhi ya watu, vikiwamo vyama vya siasa kushinikiza mabaraza ya Katiba yatumie maoni ya chama au mtu husika.

Jaji Warioba alisema hayo wakati wa kufunga mkutano wa Baraza la Katiba la Umoja wa Wabunge wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (TWPG), uliofanyika kwa siku tatu, mjini Bagamoyo, mkoani Pwani.

Alisema tangu Tume yake iiweke rasimu wazi kwa wananchi, mambo yanayojadiliwa na watu hao yamekuwa ni yale yanayohusu utawala na madaraka tu wakati rasimu hiyo imegusa meneo mengi yanayowagusa wananchi moja kwa moja, kama afya, elimu, kilimo, viwanda, biashara na ustawi wa jamii.

“Ukiangalia kwenye rasimu hii utaona kuwa wananchi wanataka uwapo wa dira ya taifa, dira ya uchumi, kisiasa na kijamii, lakini cha kushangaza mambo yanayozungumzwa ni machache tu ya madaraka. Sasa haya mengine yataboreshwaje?” alihoji Jaji Warioba.

Aidha, alivunja ukimya kuhusu mvutano unaoendelea kuhusu kipengele cha rasimu hiyo kinachopendekeza uwapo wa serikali tatu.

Alisema kipengele hicho ni maoni ya wananchi na wala si ya Tume na kusisitiza asitafutwe mchawi.

Alizitaka taasisi zote zinazotambulika na kukubalika kisheria kuwa baraza la Katiba, kufuata utaratibu mzuri wa kujadili rasimu hiyo na kuwasilisha maoni yao kwa Tume kwa kuwa haitochukua wala kuzingatia maoni yanayotolewa majukwaani.

Vilevile, alionya kampeni, ambazo alisema Tume imeanza kuzishuhudia za baadhi ya watu, vikiwamo vyama vya siasa kushinikiza mabaraza ya Katiba yatumie maoni ya chama au mtu husika, huku baadhi ya vyama vikitumia majukwaa kuwasilisha nia na maoni yao kuhusu rasimu.


“Nazungumza wazi hapa leo vyama vya siasa ni taasisi, zifuate utaratibu vijadili kama baraza la katiba la jukwaa na kutuwasilishia maoni yao, sisi kama tume hatutachukua maoni ya jukwaa wala ya kwenye helikopta,” alisema Jaji Warioba.

Alisema wakati Tume ikikusanya maoni katika eneo la elimu, wananchi walitaka shule za kimataifa zifutwe kwa kuwa zinasababisha uwapo wa matabaka ya elimu baina ya walionacho, viongozi na watoto wa wananchi wa kawaida.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, jambo hilo halileti usawa.

Alisema katika afya, pia wananchi walipendekeza safari za viongozi na wagonjwa wengine kusafirishwa nje kwa matibabu zifutwe kwa kuwa wananchi wengi wasio na uwezo hupoteza maisha katika hospitali za hapa nchini, jambo ambalo pia linasababisha matabaka.

“Sasa haya na mengine mengi kama vile kwenye kilimo, wakulima kudai kuwa wanatengwa na wafanyakazi wanapewa kipaumbele sana, ndio yanayotakiwa kujadiliwa sasa na Katiba kuboreshwa ili kupatikana Katiba itakayowahakikishia Watanzania wote usawa na haki,” alisema Jaji Warioba.

Alisema hatua iliyobaki katika kujadili rasimu ni ndogo.

Hivyo, aliwashauri Watanzania akisema huu si muda wa kulumbana, kusemezana na kutafutana wachawi, bali ni muda wa kuheshimiana na kupeana fursa ya kutoa maoni yatakayotengeneza katiba yenye manufaa kwa Watanzania wote.

Awali, Jaji Warioba alisema anategemea kuona mchago mkubwa kutoka baraza la wabunge wanawake kwa kuwa kwa kiwango kikubwa wanawawakilishwa wanawake wote Tanzania

Jaji Warioba alisema, maoni ya wabunge wanawake yatakuwa chachu kubwa kumkomboa mwanamke hususan katika masuala yanayohusu jinsia na haki za mwanamke katika

Nayo TWPG imependekeza Katiba mpya ihakikishe inazingatia haki za mwanamke kijinsia na kupiga marufuku yale yote yanayomkandamiza na kumyima haki mwanamke.

Mwenyekiti wa TWGP, Anna Abdallah, alisema walijadili rasimu ya katiba na sasa wanakusudia kuwasilisha maoni ya baraza hilo la wabunge wanawake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili ikukubali maoni na kilio cha wanawake cha muda mrefu cha uwapo wa fursa sawa katika ngazi za uongozi kwa asilimia 50/50.

“Hata hivyo, hili la ubaguzi dhidi ya wanawake, tumeona tuseme wazi kuwa tunataka litambuliwe kabisa na Katiba, kwani kwa miaka mingi tumekuwa tukiambiwa kuwa kuna usawa, lakini kimatendo suala hilo halipo,” alisema Abdallah.

Alisema baraza hilo linataka ianzishwe Tume ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Usawa wa Kijinsia, ambayo itawasilisha taarifa hizo bungeni.

Pia alisema wanataka katiba mpya itamke wazi kuwa usawa wa jinsia uwe ni moja ya tunu za taifa.

“Pia tumebainisha wazi kuwa tunataka haki za wanawake ziainishwe kwenye dibaji ya Katiba,’ alisema Abdallah.

Alisema maoni mengine ya baraza hilo ni pamoja na kutaka uchaguzi mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano uwe ndio utaratibu wa kuwawajibisha wabunge wasiotimiza majukumu yao.

Pia wanataka Katiba itambue uwapo wa mfuko wa Bunge na Tume ya Huduma za Bunge, masuala ya ardhi yabainishwe zaidi ili kuzuia umiliki holela wa ardhi kwa raia wa kigeni.

Vilevile, alisema wanataka kwenye Katiba mpya kuingizwe mtaala wa lugha ya alama katika mfumo wa elimu ngazi zote ili kurahisisha mawasiliano kwa watu wenye ulemavu.

“Tunataka katiba iweke wazi haki ya mwanamke kumiliki ardhi ikiwa ni pamoja na kurithi mali za mume wake pindi anafariki,” alisema Abdallah. 

Alisema baraza hilo katika maoni yake limependekeza Katiba itoe adhabu mbadala kwa washtakiwa wanawake wanaonyonyesha badala ya kifungo ili kulinda haki za watoto na umri wa watoto wa kike kuolewa uwe si chini ya miaka 18.

No comments:

Post a Comment