MBUNGE wa Ilemela mkoani Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), amewashutumu wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kwamba wameligeuza Bunge kuwa mzigo kwa Watanzania.
Kiwia alitoa kauli hiyo juzi wakati alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa jimbo la Ilemela katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Magomeni Kirumba, ambapo alisema adui mkubwa wa maendeleo ni serikali ya CCM.
Alisema hivi sasa wabunge wa chama tawala wameligeuza Bunge kuwa chombo kisichosikiliza kilio cha Watanzania badala yake chombo hicho kinapitisha mambo yasiyokuwa na tija kwa taifa.
Akitolea mfano wa Watanzania kuanza kutozwa kodi ya laini ya simu kwa sh 1,000 kila mwezi, mbunge huyo wa Ilemela alisema wabunge wa CCM ndiyo waliopitisha kodi hiyo bungeni.
Alisema wakati wa kujadili na kupitisha kodi hiyo ya laini ya simu, wabunge wote wa CHADEMA, hawakuwemo bungeni kwani walikuwa mjini Arusha kushiriki mazishi ya watu waliouawa kwa mlipuko wa bomu lililorushwa wakati wa kuhitimisha kampeni za udiwani.
“Bunge limegeuka kuwa mzigo kwa Watanzania. Nasema hivyo kwa sababu kuna kilio kikubwa cha Watanzania nchi nzima kuhusu kodi ya laini ya simu wanayotozwa sh 1,000 kila mwezi.
“Kodi hii imepitishwa bungeni na wabunge wa CCM. Wakati wa kupitisha kodi hii, sisi wabunge wote wa CHADEMA hatukuwemo mjengoni, tulikuwa Arusha kwenye maziko ya Watanzania wenzetu waliokufa kwa mlipuko wa bomu,” alisema Kiwia.
Aliwaomba Watanzania kuunganisha nguvu ya pamoja na CHADEMA katika harakati za kuiondoa serikali ya CCM madarakani katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu 2015 na kuipa CHADEMA dola.
“Katika utawala wa CHADEMA tunahitaji madini, maji, mbuga za wanyama, misitu, ardhi, samaki na kadhalika zimnufaishe kila Mtanzania,” alisisitiza mbunge Kiwia huku akishangiliwa na umati wa watu uliohudhuria mkutano huo.
No comments:
Post a Comment