DIWANI wa kata ya Turwa katika Halmashauri ya mji wa Tarime wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Charles Ndessi Mbusiro, amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), wilayani Tarime, kimepora uwanja wa michezo bila ridhaa ya wananchi.
Diwani huyo alitoa tuhuma hizo juzi wakati alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Tarime waliohudhuria maadhimisho ya miaka mitano ya kifo cha aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Chacha Zakayo Wangwe.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Serengeti, diwani huyo alisema kuwa uwanja huo ni mali ya wananchi wote wa Tarime lakini CCM kwa hila zake wameupora.
“Baada ya kuona uwanja huo ukitumiwa mara kwa mara na CHADEMA katika mikutano yake, wamefanya ujanja na kupata hati ambapo sasa wanadai kuwa ni mali yao.
“Ndugu zangu wananchi wa Tarime napenda kuwafahamisha kuwa uwanja huu sasa ni wa CCM, wamefanya njama na wameuchukuwa na wanadai kuwa ni wa kwao na tayari wanataka kujenga vibanda na wameshagawana vibanda kila kiongozi ana milango yake sijui kama wananchi mnalijua hilo?’’ alisema na kuhoji diwani huyo.
Diwani huyo alidai kuwa uwanja huo ulijengwa na wananchi wote kipindi cha mfumo wa chama kimoja na kwamba CCM haina hati miliki wala haina mamlaka ya kuupora.
Aliwabana viongozi wa CCM wawaambie wananchi kama chama chao ni cha biashara au ni chama cha siasa kwani viongozi wa chama hicho ndio waliojipanga kufanya biashara katika uwanja huo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa mji wa Tarime wamedai kusikitishwa na kitendo hicho ambacho walisema ni cha kifisadi na kwamba jambo hilo si la kufumbia macho.
“Unajua hawa watu wa ‘magamba’ wamezoea sana dhuluma na ufisadi; hiki kiwanja ni cha wananchi wote na wala si cha CCM sasa leo nimeshangaa kusikia kuwa wamekichukua kwa nguvu ili kiwe mali yao kwa kweli hili halitawezekana, tumechoka kuonewa liwalo na liwe lazima wakirudishe,’’ alisema mwananchi mmoja Mwita Mseti, mkazi wa mtaa wa Rebu.
No comments:
Post a Comment