CHADEMA, kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi, inatoa kauli ya awali, kulaani kitendo cha kupigwa, kuchaniwa nguo, kujeruhiwa, kunyang'anywa vifaa na kufungwa pingu kwa mwanahabari wa Channel ten, Eliah Ruzika, kilichofanywa na askari wa Jeshi la Polisi eneo la Tazara, Dar es Salaam, wakati mwandishi huyo akitimiza majukumu yake kwenye mkutano wa wafanyakazi wa Tazara.
Huu ni mwendelezo wa unyanyasaji wa raia wasiokuwa na hatia, huku wengine wakiwa katika majukumu ya kazi zao, unaofanywa na Jeshi la Polisi.
Ni mwendelezo wa askari wa jeshi hilo kunyanyasa na kuingilia wanahabari katika utekelezaji wa majukumu yao, vitendo ambavyo vimekuwa vikifanyika kwa muda mrefu sasa, hata kusababisha mauaji, bila wahusika kuchukua au kuchukuliwa hatua za kisheria, kuzuia na kukomesha kabisa udhalimu huu.
Bila shaka pia ni utekelezaji wa kauli mbovu kabisa na inayokiuka vigezo vyote vya uongozi bora, siasa safi, misingi ya demokrasia na haki za binadamu, iliyotolewa bungeni hivi karibuni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Kauli iliyoruhusu kuvunjwa kwa haki na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani kama inavyotokea sasa.
Kuminya au kujaribu kuminya utendaji kazi wa vyombo vya habari na wanahabari, ni hatua ya juu sana kuelekea kuminya haki na uhuru wa kufikiri na kutoa maoni, kwa mtu mmoja mmoja, kundi au makundi ya watu katika jamii.
Kuminya uhuru na haki ya habari na kutoa maoni, huku ukitegemea polisi kutawala (kwa kuigeuza nchi police state) ni moja ya dalili za mwisho mwisho ya watawala waliochoka, wanaotakiwa kupisha madarakani.
Kurugenzi ya Habari CHADEMA
No comments:
Post a Comment