Friday, August 2, 2013

Marando: Tulikosea kukurupukia majina

MWANASISASA maarufu chini, Mabere Marando, amesema kuwa Chama chake cha zamani cha NCCR-Mageuzi kilifanya makosa, kwa kukurupukia majina makubwa katika miaka ya mwanzo ya mageuzi.
Marando ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa NCCR–Mageuzi, alisema hayo katika mkutano wa vijana chini ya mwamvuli wa ‘International Young Democrat Union (IYDU)’ ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni mwanachama.
Mkutano huo ulifanyika Tanzania chini ya uenyeji wa CHADEMA na kudhaminiwa na taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS).
Akizungumza na Tanzania Daima, Marando ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, alisema CHADEMA walikuwa makini kwa kuwapokea waliojiunga na chama chao, hali iliyosaidia kuwa na nguvu ya kisiasa hadi leo.
“Sisi (NCCR) tulikurupuka, hasa Augustine Mrema, alipojiunga na chama chetu tukamkabidhi wadhifa wa uenyekiti bila kuangalia athari za kuwa na mtu maarufu kuliko chama chetu,” alisema.
Hata hivyo alikiri kuwa migogoro imekuwa na manufaa ya ziada kwa kuwafanya wapinzani wakomae na sasa wana uwezo wa kuwachuja wabaya bila kuathiri uhai wa vyama vyao.
Akifafanua zaidi alisema vyama vya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) viliponzwa na mikakati ya chama tawala ikiwamo kuvipakazia kuwa ni vya kikabila na udini, hasa CUF kilichodaiwa kupigania masilahi ya Waislamu kuliko mustakabali wa maendeleo ya nchi.
Akizungumza kwa kujiamini, Marando alisema mikakati kama hiyo haiwezi kuidhoofisha CHADEMA kwa sababu wananchi wamefunguka na kamwe hawataathiriwa na propaganda uchwara zinazoenezwa na wapinzani wao.
Naye mwandishi wa habari nguli, Jenerali Uliwengu, alisema Tanzania imepoteza ‘viongozi’ na sasa ina ‘wababaishaji’.
“Inashangaza kusikia mtu mzima akisema sasa tumechoka tutawapiga tu, kama amechoka si ajiuzulu awapishe wenye nguvu? Kwa nini anaanza kupiga wenzake hovyo hovyo?” alihoji Jenerali.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria (Tanganyika Law Society), Wakili Francis Stolla, alisema Watanzania wanapaswa kuenzi mchango wa wanamageuzi wa awali ambao walikutana na misukosuko mingi bila kuchoka.
Alisema mazingira ya sasa yanatoa mwanya wa wananchi kutoa madukuduku yao bila woga kama ilivyokuwa mwanzoni mwa miaka ya 90 uliporuhusiwa mfumo wa vyama vingi.

No comments:

Post a Comment