Friday, August 2, 2013

CHADEMA wajipanga kumng’oa meya

MBUNGE wa Ilemela, mkoani Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), ametangaza kuongoza maandamano makubwa wiki ijayo kwa ajili ya kumng’oa Meya wa manispaa hiyo, Henry Matata, aliyechaguliwa kinyume cha kanuni.
Matata ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri, alichaguliwa kuwa meya wa manispaa hiyo Septemba mwaka jana, katika mkutano ambao ulikuwa haukidhi akidi ya madiwani 14, ambao ni kwa mujibu wa sheria.
Meya huyo aliyevuliwa uanachama wa CHADEMA mwaka jana kutokana na kusababisha mgogoro ndani ya chama mkoani Mwanza, alifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo lakini wakati kesi hiyo bado ikiendelea alichaguliwa kuongoza manispaa hiyo mpya iliyomegwa kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Kwa mujibu wa sheria za halmashauri hiyo, akidi ya wajumbe wanaohitajika kwa ajili ya kumchagua meya ni madiwani tisa lakini Matata alichaguliwa na madiwani sita pekee, wanne wa CCM na mmoja wa CUF bila madiwani wanane wa CHADEMA kuwapo.
Akizungumzia sakata hilo la meya kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Magomeni juzi, Kiwia alisema kuwa maandamano hayo yataungwa mkono na wananchi wa Nyamagana, ambapo wataweka kambi katika makao makuu ya ofisi za wilaya hiyo.
Kiwia alisema kuwa yeye, madiwani na viongozi wengine wa CHADEMA wamelazimika kuandaa maandamano hayo kwa lengo la kwenda kudai haki dhidi ya nafasi ya meya ambaye hawamtambui na kwamba anashikilia nafasi hiyo kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, maandamano hayo yatafanyika Alhamisi wiki ijayo kwa wananchi kuweka kambi ofisi za mkuu wa wilaya hiyo, kushinikiza Matata kuondolewa kwenye nafasi hiyo.
"Matata alichaguliwa na madiwani sita kati ya14 wa manispaa ya Ilemela ambao ni wajumbe halali. Uchaguzi huo ulikuwa batili maana haukufikia theluthi mbili ya wajumbe tisa wanaohitajika”.
“Licha ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza, kuwa kiongozi anayepaswa kusimamia sheria za nchi na kanuni zake, yeye pamoja na wanasheria waliruhusu uvunjifu wa sheria kwa Matata kuchaguliwa na madiwani sita kati ya 14,” alisema.
Kiwia alisema wanatangaza kufanya maandamano makubwa ambayo hayajawahi kutokea kwa ajili ya kwenda kudai haki yao.
Hata hivyo, mbunge huyo alilituhumu vikali Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, serikali na chama tawala kwa madai kwamba wapo nyuma ya Matata, kwani licha ya kuchaguliwa kinyume cha sheria na kumtishia maisha, hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alisema kuwa baada ya Matata kuchaguliwa kinyume cha sheria, CHADEMA waliwasilisha pingamizi na malalamiko yao kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, wakipinga uchaguzi huo, lakini hadi sasa serikali imekaa kimya.
“Tulipeleka pingamizi kwa Waziri Mkuu, Pinda na Hawa Ghasia, tukipinga uchaguzi huo batili lakini mpaka leo hii wamekaa kimya. Hii inaonesha kuna viongozi wa serikali na CCM yao wapo nyuma ya Matata,” alisema.
“Sasa tumechoka, tunataka haki itendeke. Alhamisi nitakuwapo pamoja na Ezekiel Wenje wa Nyamagana na Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli, katika mkutano kwa ajili ya maandamano,” alisema.
Kuhusu kutishiwa kuuawa na Meya Matata mbele ya Mkuu wa Wilaya, Amina Masenza na askari polisi bila kuchukuliwa hatua, Kiwia alihoji kama kiongozi huyo yupo kwa masilahi ya wananchi au CCM.
Alisema kuwa haiwezekani mtu anasimama mbele ya mkuu wa wilaya na kutoa vitisho vya kuua, lakini kiongozi huyo ambaye ni mlinzi wa amani wilayani kwake akakaa kimya.
Awali, Diwani wa chama hicho Kata ya Nyamanoro, Abubakari Kapera, alimtaka Rais Jakaya Kikwete amfukuze kazi mara moja Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kwa madai kwamba ameshindwa kusimamia haki na amani wilayani humo.
Alisema kuwa kitendo cha mkuu huyo kushindwa kumkamata Matata wakati akitoa vitisho kwa mbunge wao, mbele yake kikaoni, inaonesha wazi kwamba kiongozi huyo hajui wajibu wake.

No comments:

Post a Comment