TANZANIA imetakiwa kutoharakisha kutumika Katiba mpya ili kuepuka kasoro zinazoweza kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKITA), Deus Kibamba, ikiwa ni siku chache tangu arejee nchini kutokea Zimbawe kufuatilia mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Julai 31, mwaka huu chini ya katiba mpya.
Kibamba aliyeongozana na wenzake, alisema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro nyingi zilizotokana na kuharakishwa kwa katiba ya nchi hiyo na kusababisha baadhi ya wananchi na vyama vya siasa kukosa haki za msingi.
“Haiwezekani mkamilishe kuandika katiba mpya juzi, leo ianze kutumika bila kupitia na kutafsiri sheria zilizopitishwa humu … lazima mtachemsha tu kama walivyofanya Wazimbabwe katika uchaguzi wao, maana kasoro nyingi zilijitokeza katika tafsiri,” alisema.
Alisema baadhi ya kasoro zilizojitokeza katika kipindi hicho hasa zilizoilenga Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC) ni pamoja na suala la uandikishaji wapiga kura, ambapo walidai kuwa vituo vilikuwa vichache na siku zikawa chache.
Kasoro nyingine ni daftari la wapiga kura kuwa la kata nzima badala ya kituo husika ili kuepusha wananchi kupiga kura zaidi ya moja, kutoweka daftari la kuwekwa wiki moja kabla ya kupiga kura ili wananchi waweze kushuhudia majina yao kama yapo au la.
Serikali kuchelewa kupeleka fedha kwa ajili ya zoezi la kupiga kura, hali iliyochangia vifaa visifike katika vituo siku moja au mbili kabla ya upigaji kura; huku kundi maalumu la askari nchini humo ambalo lilipiga kura wiki mbili kabla ya wananchi, nalo kurudia kupiga kura.
Kibamba alisema kasoro hizo na nyingi ambazo hajazitaja zilisababishwa na uharaka wa kuandika na kuanza kuitumia katiba mpya ya nchi hiyo.
Aidha, Kibamba alivitaka vyama vya upinzani hapa nchini viungane na kukubaliana kusimamisha wagombea ili kuweka nguvu ya pamoja ili viweze kushika dola, vinginevyo utakuwa mgumu kwao.
“Funzo jingine nililolipata katika uchaguzi wa Zimbambwe na ule wa Kenya ulioisha ni kwa vyama vya siasa kuungana ili viwe na nguvu moja ya kushinda … bila nguvu ya pamoja, chama kinachotawala hakitaweza kutoka madarakani,” alisema Kibamba.
Alisema hatashangaa kuona matokeo ya urais kwa vyama vya upinzani nchini Zimbambwe yanakuwa mabaya kutokana na kutoungana na kutoaminiana kwao.
Kibamba alitaka Tanzania iige Kenya ambayo mchakato hadi kupatikana kwa katiba yake ulikwenda polepole, ukamalizika na uchaguzi ukafanyika ndani ya miaka miwili baada ya kupatikana.
Naye Mkuu wa jopo la msafa wa waangalizi wa Jukwaa hilo, Asha Aboud Mzee, alisema waangalizi wa makundi mbalimbali kutoka SADC, AU na NGOs za Afrika walisaidia baadhi ya migongano iliyojitokeza katika kampeni hadi upigaji kura.
“Kwa mfano Chama cha MDCT cha Morgan Tsvangirai kilipokataliwa kufanya kampeni yake ya mwisho Julai 29 mwaka huu kutokana na msaada wa waangalizi, chama hicho kiliruhusiwa na ZEC kufanya kampeni yake,” alisema.
No comments:
Post a Comment