Sunday, August 4, 2013

Dk. Slaa ampa JK ushauri adhimu

 ASEMA HERI KUPATANISHA KAGAME NA WAASI KULIKO KUTAKA ‘WAYAMALIZE’
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema Rais Jakaya Kikwete alipaswa kuwapatanisha Rais Paul Kagame na waasi wa FDLR badala ya kumtaka rais huyo wa Rwanda akutane na waasi hao, jambo ambao limeibua hisia hasi na kuhatarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Alisema haoni mantiki ya Rais Kikwete kumtaka Rais Kagame akae na wafuasi wa FDLR, wakati yeye mwenyewe ndani ya nchi yake akishirikiana na Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda, wameviagiza vyombo vya dola kuwapiga wapinzani.
“Rais Kikwete anakosa mamlaka ya kimaadili ya kumwambia Kagame atekeleze kitu ambacho yeye mwenyewe hatekelezi nchini kwake. Yeye alipaswa kumwita Kagame na waasi ili awapatanishe. Ni vigumu kuwaambia watu waliopigana na kuuana kaeni meza moja mzungumze. Badala yake yeye, kama alikuwa na nia njema, angewaita na kuwapatanisha,” alisema.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam baada ya kutakiwa kutoa maoni yake juu ya hotuba aliyoitoa Rais Kikwete juzi. Alisema uhusiano wa Rwanda na Tanzania unapita katika kipindi kigumu kutokana na viongozi hao kutoleana maneno yasiyofaa.
Dk. Slaa alisema Rais Kikwete hivi sasa anapaswa kukutana na Rais Paul Kagame wazungumze na kumaliza tofauti zao ili kuepusha nchi zao kuingia kwenye vita.
Alisema kama viongozi hao hawatachukua hatua madhubuti na maneno baina yao yakaendelea, kuna kila dalili ya kuzuka kwa vita baina ya mataifa haya mawili siku za usoni.
“Mimi sipendi nchi zetu ziingie vitani kwa sababu ya kauli za viongozi wawili, hapa tunazungumzia kushambulia na kushambuliwa, hawa marais wawili wangekutana kumaliza tofauti zao, maana wananchi wa mataifa haya ni ndugu,” alisema.
Akitoa hotuba ya mwisho wa mwezi, Kikwete alisema: “Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano kati ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo.”
Katika hotuba yake ya juzi, Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miezi miwili kuanzia Mei mwaka huu, uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda unapitia katika wakati mgumu kutokana na kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yake.
Hata hivyo Rais Kikwete aliwahakikishia Watanzania kuwa serikali anayoiongoza inapenda kuwa na uhusiano mzuri na nchi zote jirani, kwa sababu kila mmoja anamhitaji mwenzake, hivyo lazima uhusiano na ushirikiano mwema uendelezwe.
Slaa apinga utoaji wa fedha
Katika mkutano wake wa ufunguzi kwa BAVICHA, Dk. Slaa alisema serikali imekuwa ikitoa fedha kwa Watanzania kama karanga badala ya kuwekeza kwenye ajira za vijana.
Alisema serikali imetumia zaidi ya sh bilioni saba kulipa posho na tiketi za ndege kwa ajili ya baadhi ya wageni waliotoka nje kuja kuhudhuria mkutano wa ‘Smart partnership’ na tangu ufisadi huo ufanyike hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
“Rais wetu anagawa fedha za nchi kama njugu kujitafutia umaarufu badala ya kuwekeza kwa vijana ili kupunguza tatizo la ajira ambalo tumekuwa tukilizungumzia kila mara, uchumi wetu upo mahututi (ICU), lakini tunakubali kupoteza mabilioni kwa ajili ya kujipendekeza, Rais Obama alipokuja nchini tulipoteza pesa nyingi sana, lakini sisi Watanzania tumepata nini? Tujiulize.
“Rais wetu amewahi kutoa shilingi trilioni 1.7, siku tatu kabla ya kikao cha bajeti, kinyume kabisa cha utaratibu, lakini hao wameshazoea, na ndiyo maana mapendekezo ya CCM kuhusu rasimu ya Katiba mpya yanakataza uwazi na uwajibikaji,” alisema.
Dk. Slaa alisema Rais Kikwete alitangaza kutoa sh bilioni moja kila mkoa, lakini mpaka hivi sasa watu waliozipata fedha hizo ni wachache kuliko kiwango kilichotolewa, jambo linalozua utata kuwa zimeishia mifukoni mwa wajanja wachache.
Awaasa vijana
Dk. Slaa alisema adui wa kwanza wa uchumi wa Tanzania ni elimu duni na vijana wamekuwa wakipata elimu hiyo ambayo imeshindwa kuwasaidia kujitegemea na kujiajiri.
Aliongeza kuwa Chadema wanahitaji kubadili mfumo wa elimu na kuufumua ili uendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, hivyo kufungua fursa za kujiajiri.
“Nawaasa vijana mfanye kazi kwa bidii, acheni kulalamika juu ya ugumu wa maisha, uongozi mbaya na mambo mengineyo yaliyopo kwenye jamii, vijana mmepata hasara kwa kutozingatia muda,” alisema.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki, Dk. Kamilius Kasala, ameukosoa mpango wa kukuza pato kuelekea mwaka 2025, ambapo alisema matazamio ya serikali hayawezi kuwa na matunda ifikapo mwaka huo, kwakuwa takwimu zinaonyesha thamani ya fedha inazidi kuporomoka na kutengeneza uchumi tegemezi.

No comments:

Post a Comment