HALI ya ubadhirifu wa fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuishia kwenye mikono ya watendaji wasiokuwa waaminifu ndiyo fimbo ya kukiangamiza Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAA), Rajab Mbarouk, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ole, Kaskazini Pemba (CUF), alieleza hayo jana wakati wa kikao cha majumuisho kilichofanyika mkoani hapa.
Mbarouk alisema CCM haiwezi kudumu madarakani na yupo tayari kuiona ikifa wakati wowote kutokana na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma unaofanywa na watendaji wake, huku Mkoa wa Mbeya ukiongoza kwa utovu wa nidhamu na kuwa na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho baada ya kukamilika kwa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo uliofanywa na kamati hiyo kwenye halmashauri nne za mkoa huo alisema: “Natamani hata sasa hivi CCM itoke madarakani, iondoke, kwa sababu watendaji wake wanataka CCM iondoke madarakani na chama changu kichukue nchi, natamani lakini najua watakaofanya iondoke madarakani ni wananchi kwa kutumia sanduku la kura, haiwezekani wananchi waibiwe hivi.”
Akisoma taarifa iliyotolewa na kamati hiyo mbele ya Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Deodatus Kinawiro, mjumbe wa kamati hiyo, Geofrey Zambi, alisema Mbeya ndiyo inaongoza kwa utovu wa nidhamu nchi nzima kwa kuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali huku Wilaya ya Mbarali ikiongoza kwa ubadhirifu wa fedha baada ya kutumia kiasi cha zaidi ya sh milioni 800 zilizoingizwa kimakosa na Hazina kwenye akaunti ya halmashauri hiyo.
Taarifa hiyo ambayo inaonesha kuuma na kupuliza iliweza kubainisha wazi namna fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinavyotafunwa kupita kiasi na watendaji wa serikali na asilimia ya matumizi kutofautiana na hali halisi ya fedha zilizotumika kwenye miradi hiyo.
“Kama Mwenyekiti wa CCM mkoa lazima tukubali haya yaliyosemwa, tukifanya vibaya CCM tunawapa mahali pa kusemea, si Chama Cha Mapinduzi kinachokula hizo fedha isipokuwa wataalamu ndio wanatuangusha, watumishi wamewazidi ujanja madiwani na hao ndio wanaosema serikali ya Chama Cha Mapinduzi haina lolote kumbe wao ndio wanatuibia,” alisema.
No comments:
Post a Comment