CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepanga kutumia helikopta kuzunguka jimbo la Arumeru Magharibi la Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodlucky ole Medeye kwa lengo la kumshtaki kwa wapiga kura wake.
Chama hicho kinadai kuwa kitendo chake cha kuhamasisha ubaguzi wa kikabila ndani ya jiji la Arusha wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani hivi karibuni hakikubaliki.
Pia CHADEMA imelitaka Jeshi la Polisi kuacha kuwasumbua kwa kuwapiga na kuwabambikizia kesi za uongo wanachama wake.
Rai hizo zilitolewa juzi na Katibu wa CHADEMA kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, akiwa na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya Sekondari Ngarenaro kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa ushindi wa viti vinne vya udiwani.
Golugwa alisema kuwa wanajua wajibu na umuhimu wa jeshi hilo katika kusimamia usalama na mali za raia, hivyo watekeleze majukumu yao kwa weledi na wawaheshimu viongozi na wanachama wa CHADEMA wakielewa kuwa ni chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria na kinachoendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
“Ninawaomba polisi tuheshimiane hapa mjini, kwani hata sisi ni chama cha siasa chenye haki sawa na chama kingine chochote chenye usajili wa kudumu, hakuna sababu ya kupigana na kutengenezeana kesi zisizo na sababu,” alisema.
Alisema kuwa wakati jeshi hilo likihimiza utii wa sheria bila shuruti lenyewe limekuwa likitenda kinyume cha kauli mbiu hiyo kwa kutoa kauli zisizo za kweli kama ile ya Kamanda wa Polisi Mkoa, Liberatus Sabas, na Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, kudai kuwa wapelelezi toka nchini Marekani (FBI) wako Arusha kuchunguza tukio la mlipuko wa bomu.
“Walisema FBI wako Arusha kuchunguza tukio la bomu lililoua watu wanne na kujeruhiwa wengine zaidi ya 70, tukashangaa muda unaenda mbona waathirika hatuhojiwi ikabidi viongozi wetu wawasiliane na ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam wakaambiwa hakuna FBI waliofika nchini,” alisema.
Akihutubia mkutano huo, Lema alisema kuwa CHADEMA imejipanga kumshtaki Ole Medeye kwa wapiga kura wake kutokana na kitendo chake cha kusimamia kikao kilicholenga kuwahimiza watu wa kabila la Kimasai kuyabagua makabila mengine yalioko Arusha.
Alisema kuwa kwa dhambi hiyo aliyoifanya Medeye ni lazima wakamshtaki kwa waliomchagua ambapo alidai kuwa wametenga sh milioni 38 kwa ajili ya kuweka mafuta kwenye helikopta atakayozunguka nayo kwenye jimbo hilo.
Siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa madiwani, baadhi ya wazee wa kimila wa Kimasai wakiwa na Ole Medeye walikutana eneo lao la matambiko ndani ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambapo miongoni mwa mambo waliyoazimia ni kuhakikisha watu wasio wa asili ya Arusha hawachaguliwi kwenye uchaguzi huo.
Naye kada wa chama hicho, James Millya, alielezea masikitiko kwa kitendo cha serikali kuwathamini wawekezaji wa nje kuliko wazawa ambapo alitolea mfano kuwa hivi karibuni yalitokea mauaji kwenye mgodi wa kampuni ya Tanzanite One baada ya kutokea kile kinachoitwa ‘mtobozeano’.
No comments:
Post a Comment