Saturday, July 13, 2013

Waziri apanga kuvuruga uchaguzi Arusha

MGOMBEA WA CHADEMA AKAMATWA USIKU WA MANANE 
NJAMA za kutaka kuvuruga uchaguzi mdogo wa marudio wa madiwani unaotarajia kufanya kesho jijini Arusha, zimekwama baada ya kundi lililoitwa kupewa mikakati ya kushiriki vurugu hizo kugoma.
Mbali na njama hizo, zilizokuwa zikiratibiwa na naibu waziri mmoja (jina linahifadhiwa), juzi usiku askari polisi wanaoaminika kutumwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), walimkamata mgombea udiwani wa CHADEMA, Kata ya Kimandolu, Raisoni Ngowi nyumbani kwake na kumpeleka kulala rumande kabla ya kuachiwa asubuhi.
Habari za kuaminika zimebainisha kuwa Naibu Waziri huyo jana aliratibu na kisha kukutana na wazee wa kimila wa kabila la Kimasai kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha na Manyara, na kuwataka wawaagize vijana wote wa Kimasai kufanya maandamano makubwa na vurugu ili kusaidia kutofanyika kwa uchaguzi wa Jumapili.
Hatua hiyo kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, ililenga kuzuia kufanyika kwa mara nyingine uchaguzi huo, kutokana na kile kilichoelezwa kuwepo kwa ‘upepo mbaya’ kwa upande wa wagombea wa CCM.
Imedaiwa kwamba awali wazee hao wa kimila waliitwa katika Ukumbi wa Arusha Technical College, wakiambiwa kuwa ni kikao cha kujadili mambo ya mila, lakini wakashangaa walipoanza kupewa mkakati huo mchafu na naibu waziri huyo.
Habari zinasema kuwa naibu waziri huyo aliwaambia wazee hao wafanye wawezalo kwa mamlaka na heshima kubwa waliyonayo, kuwaamrisha vijana wao kuandamana kupinga matendo ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwamba amevunja mila za kabila hilo kwa sababu ni Mchaga na hivyo, hawapo tayari kuruhusu wagombea wengine wanaopigiwa chapuo na CHADEMA katika mkoa wao.
Hata hivyo, katika hali ya mshangao, wazee hao maarufu kama Laigwan, walimpinga na kukataa hoja hizo za mtendaji huyo wa serikali. Walimwambia kuwa hawawezi kujiingiza katika mchezo huo mchafu wa ubaguzi wa kikabila kwa sababu, hata miongoni mwa Wamasai, wapo wengi waliooa ama kuolewa na Wachaga na makabila mengine.
“Huo ni mchezo mbaya sana, maana hata sisi tumeoa kwa Wachaga na makabila mengine, na tumehamia sehemu nyingine na wengine nje ya nchi,” alisikika akisema Laigwan mmoja katika kikao hicho.
Wazee hao walizidi kumpa ukweli waziri huyo mdogo, wakimtaka ajue kuwa kazi za wazee hao ni kushughulikia mambo ya kimila na kuwafunda vijana wao maadili mema na sio kuwalisha siasa na mambo ya ovyo.
Naye Mwandishi Ramadhan Siwayombe anaripoti kuwa mgombea udiwani wa CHADEMA, Kata ya Kimandolu, Ngowi alikamatwa nyumbani kwake na kulala rumande kabla ya kuachiwa asubuhi.
Kukamatwa huko kwa mgombea kunatokea wakati kukiwa na malalamiko ya mabalozi wa nyumba kumi kuzunguka kukusanya shahada za wapiga kura na kuzinakili bila kufahamu ni kwa ajili gani.
Akizungumzia tukio hilo kwa Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema kuwa wameshangazwa na kitendo cha polisi kumkamata mgombea huyo usiku wa saa 7.00 nyumbani kwake.
Alisema kuwa mgombea huyo akiwa nyumbani kwake Kimandolu amelalala, huku walinzi wa chama chake, Red Brigade wakimlinda, walishitukia polisi wanavamia nyumbani hapo na kumkamata yeye na walinzi hao na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi.
Alifafanua kuwa mara baada ya kuwafikisha kituoni waliwaweka rumande hadi jana asubuhi, kisha walimuachia Ngowi pekee na walinzi wake kuendelea kuwashikilia.
“Sisi tunaamini Mungu anashuhudia hayo yote na ataleta neema yake na uchaguzi huu tutashinda kwa kishindo licha ya hujuma mbalimbali zinazoendelea kufanywa dhidi yetu,” 'alisema Golugwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi alipotafutwa kuzungumzia kamatakamata hiyo hakupatikana na alipopigiwa simu yake ya mkononi alisema yupo katika maandalizi ya mapokezi ya Rais Jakaya Kikwete, hivyo hayupo katika nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo.
Uchaguzi wa kata hizo unatarajiwa kufanyika kesho, baada ya madiwani wanne wa CHADEMA kufukuzwa  uanachama. Madiwani hao na kata zao kwenye mabano ni  Estomiah Mallah (Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles Mpanda ‘Rasta’ (Kaloleni).
Wagombea waliopitishwa na CHADEMA kugombea katika kata hizo katika uchaguzi wa kesho na kata zao kwenye mabano ni Emmanuel Kessy (Kaloleni), Jeremia Mpinga (Elerai), Malance Kinabo (Themi) na Rayson Ngowi (Kimandolu).
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha akiongea na wanahabari kuhusiana na uchaguzi huo, alisema lazima utafanyika na ulinzi umeimarishwa na Jeshi la Polisi kuhakikisha unaisha salama.

No comments:

Post a Comment