Saturday, July 13, 2013

CHADEMA yamuanika JK, CCM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa hadharani kinachoweza kuitwa ‘ushahidi’, kikionyesha namna Rais Jakaya Kikwete na viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walivyohusika na shughuli za kijeshi zinazofanywa na vijana wa chama hicho maarufu kama Green Guard.
Mbali na kufichua hali hiyo, CHADEMA pia kimemtaka Rais Kikwete na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema kukifuta kwanza kikundi hicho cha vijana wa CCM na makambi aliyodai yanaendeshwa kijeshi, badala ya kuwashutumu kwa maneno makali CHADEMA.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Oganizesheni na Mafunzo, Benson Kigaila alisema CHADEMA wanashangazwa na kauli za vitisho za viongozi hao, huku wakijua kuwa kuna makambi ya CCM ambayo yamekuwa yakifanya mafunzo ya kijeshi.
Kigaila alisema Rais Kikwete aliwahi kuhudhuria mafunzo ya aina hiyo yaliyofanyika jijini Mwanza mwaka 2012, na kupigiwa saluti.
“Kabla ya kunyoosha kidole kwa mwingine, ni vyema kwanza viongozi hao wakaliondoa boriti lililopo katika jicho lao…kwani wamekuwa wakifanya mafunzo ya kijeshi, tena Rais Kikwete anajua na IGP anafahamu hilo, lakini hakuna aliyekamatwa wala kuchukuliwa hatua,” alisema.
Alisema kutokana na mafunzo hayo, CHADEMA wanaamini vijana hao wa CCM ndio waliohusika kuwadhuru na kuwajeruhi wabunge Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatory Machemli wa Ukerewe – wote wa CHADEMA.
Mkuu huyo alisema kuwa pamoja na vijana wa CCM kuendesha vurugu hizo na hata kutumia silaha, sio Rais Kikwete wala wakuu wa vyombo vya dola waliowahi kutoa tamko.
Alisema CCM iliendesha mafunzo katika makambi yaliyojumuisha vijana 500 jijini Mbeya na vijana kupelekwa mkoani Iringa katika Kata ya Kibete na Mbalamaziwa na kutenda uovu na hadi sasa hakuna aliyekamatwa.
“Tunapenda kama kweli viongozi hao wana nia ya dhati ya kutokomeza hili, waanze na Mbunge wa Iramba, Mwigulu Nchemba. Huyu ndiye amekuwa kinara wa kuwaweka vijana hao katika makambi na tumekuwa tukitoa taarifa polisi, lakini hakuna utekelezaji unaofanyika,” alisema Kigaila.
Alisema kuwa pamoja na kutoa malalamiko ya kuwepo kwa kambi hizo za kijeshi, lakini viongozi wa chama tawala wamekuwa wakijitetea na kusema mafunzo hayo ni ya ujasiriamali.
Aidha, Kigaila alionyesha baadhi ya picha ambazo zimepigwa katika maeneo ya makambi ya vijana wa CCM huku wakiwa wamebeba silaha na nyingine zikionyesha Rais Kikwete akipigiwa saluti.
“Hivi leo kama mnatoka kupewa mafunzo ya ujasiriamali hivi unabeba silaha kwa ajili ya nini na wakazitumie wapi?” alihoji.
Kiongozi huyo alisema kuwa ni vyema Jeshi la Polisi likaanza na CCM na kuepuka kutazama jambo hilo kwa jicho moja kwa kuwa CHADEMA itakuwa ya mwisho kuchezea amani ya nchi.
“Watuambie ni wapi CHADEMA ilifanya vurugu, maana sisi tuna ushahidi uliofanywa na CCM…ni vyema Jeshi la Polisi likaepuka utawala wa kulindana ambao unaongozwa na kufanywa na CCM hatua inayosababisha kufanya madhambi,” alisema.
Alisema kuwa CCM ndiyo watakuwa wa kwanza kuipeleka nchi sehemu mbaya kutokana na polisi kushindwa kuwachukulia hatua watawala hao.
“Hawa watu wanaenda mafunzoni wana bunduki kabisa, lakini tumekuwa tukisema na kuambiwa kuwa ni matoi,” alisema Kigaila.



UVCCM wajikanyaga
Katika hatua nyingine, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umekiri kumiliki kikundi cha vijana wanaojifunza ukakamavu (Green Guard) kwa madai ya kutoa ulinzi katika shughuli mbalimbali za chama hicho.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Martin Shigela alilazimika kutoa kauli hiyo, baada ya kubanwa na waandishi wa habari aliokutana nao jana katika makao makuu ya umoja huo, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Shigela ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alidai kuwa hakuna mafunzo ya kijeshi wala silaha wanayopewa vijana hao, bali wanafundishwa ukakamavu na kujilinda katika shughuli za chama hicho.
Alisema mafunzo kwa vijana wao ni kwa ajili ya mahitaji ya sherehe, gwaride la ukakamavu na matamasha mengine na sio silaha kama ilivyodaiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kabla ya kukiri jambo hilo, Shigela alianza kumshambulia Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwa tamko lake la kuanzisha kambi nchi nzima kwa ajili ya kuwapa mafunzo maalumu walinzi wa chama hicho, Red Brigade, ili kuwalinda viongozi na wanachama wake.
Katika tamko lake, Mbowe alisema CHADEMA imeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuongezeka kwa mashambulizi, kutekwa, kujeruhiwa na hata kuuawa kwa wanachama wake na viongozi, huku serikali ikishindwa kuchukua hatua za usalama.
Hata hivyo, hatua ya CHADEMA ilijibiwa kwa ukali na vyombo vya dola na viongozi wa CCM na serikali, kwamba ni ukiukwaji wa sheria.
Jana, Kigaila aliwataka Watanzania kuepuka propaganda zinazofanywa na viongozi wa CCM ya kupenda kupotosha masuala mbalimbali yanayohusiana na kikosi hicho.
“Sisi hatuanzishi kikundi cha kijeshi bali tunakwenda kuwapa mafunzo vijana wetu ili waweze kuwalinda viongozi na wananchi pindi wawapo katika mikutano,” alisema Kigaila.
Alisema mafunzo yao hawatakuwa na silaha na watatangaza baadae mikoa watakayoenda na muda wa mafunzo hayo.
Kigaila alisema kuwa katiba ya chama chao imeruhusu kuwa na vijana na imesajiliwa kikatiba.

No comments:

Post a Comment