MBUNGE wa Ubungo John Mnyika (CHADEMA) amesema kuwa hataacha kufanya siasa kwenye suala la tozo za kadi za simu hadi pale kodi hiyo itakapofutwa ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha.
Mnyika alifikia kutoa kauli hiyo baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, kueleza kuwa mbunge huyo amekuwa akichukua uamuzi huo baada ya kuona malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Mnyika anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili.”
Kwa mujibu wa taarifa aliyotoa jana katika mitandao ya kijamii, Mnyika alisema kuwa hawezi kuacha kufanya siasa kwa sababu ndio kazi aliyopewa na wananchi ya kutakiwa kuisimamia serikali.
“Wananchi walinichagua kuifanya kazi ya kuwawakilisha na kuisimamia serikali ambayo yeye Makamba ni sehemu yake.
“Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora,” alisema.
Alisema kuwa jambo ambalo hawezi kulifanya ni siasa chafu kama hizo zinazofanywa na Makamba za kusema uongo.
Mbunge huyo alisema kuwa hajaanza kuongea kuhusu suala hili baada ya kutolewa kwa malalamiko ya wananchi bali alianza kulishughulikia tangu bungeni baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi Dk. William Mgimwa kuwasilisha jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu ikiwemo hiyo.
“Katika mchango wangu bungeni, nilieleza kwamba muswada huo wa sheria ya fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada wa majanga ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha wananchi’.” Alisema.
Alisema hakuishia kusema bali alichukua hatua kwa mujibu wa kanuni za Bunge ambapo aliwasilisha jedwali la marekebisho ya kupinga kodi ya umiliki wa kadi za simu pamoja na kodi nyingine zote zenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha.
Aidha Mnyika aliwataka wananchi kumhoji Makamba kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu na kwenye mitandao ya kijamii ambapo alitoa namba ya mkononi ya simu ya kiongozi huyo (ambayo imehifadhiwa).
“Kwa kuwa yeye ni sehemu ya serikali na ndiyo ambayo iliingiza suala hili kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge kupitia hotuba ya Bajeti ya Serikali na ikalirudia kuliingiza kupitia jedwali la marekebisho ya sheria ya serikali, ni kina nani hasa kwa majina ndani ya serikali na Bunge walioingiza kodi hii? Na ni kina nani hasa waliopigia kura ya kuipitisha?” alihoji na kuongeza: “Huyo Makamba anaeleza kwamba hakubaliani na suala hili na kupita kwake ilikuwa ni kuzidiwa nguvu, ataje kwa majina hayo walioizidi nguvu serikali kinyume na matakwa yake,” alisema.
Alisema kuwa Makamba alinukuliwa akisema kwamba anajua kuwa suala hili haliwezi kutekelezwa na kwamba ni lazima litabadilishwa kwa kuangalia eneo lingine la kutoza kodi.
“Ni vizuri akahojiwa, ikiwa huo ni msimamo wa serikali; mwenye mamlaka ya kusitisha kodi hiyo ni nani na kwa nini hajitokezi kutoa agizo la kusitisha wakati maandalizi yakiendelea ya kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa kodi hiyo katika mkutano ujao?” alisema.
Wakati Naibu Waziri akisema hayo, Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa katika serikali hiyohiyo yeye ametoa kauli tofauti siku hiihii ya leo ambapo kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania amewataka watumiaji wa mitandao ya simu nchini na Watanzania kwa ujumla kuwa na subira kuhusu tozo ya sh 1000 kwa mwezi kwa kila laini ya simu za kiganjani.
Alisema kuwa kauli za ujumla zinazotolewa na serikali bila kuwataja kwa majina wahusika ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hiyo na nyinginezo ambapo wanahamisha mzigo huo kwa wabunge.
“Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Rais au kiongozi mwingine mwenye mamlaka, ajitokeze kusitisha kutozwa kwa kodi hiyo na kuanzisha mchakato wa muswada wa kufuta kodi hiyo utakaowasilishwa katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza Agosti 27, mwaka huu,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment