MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), anatarajia kufanya mkutano wa kihistoria katika mji wa Mbalizi, wilaya ya Mbeya Vijijini kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo, Kissman Mwangomale, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mshikamano kata ya Nsalala, alisema mkutano huo utafanyika katika viwanja vya mahubiri vilivyoko Tazara mjini hapo.
Alisema ziara hiyo ya Lema imeandaliwa na kata mbili ambazo ni kata ya Utengule Usongwe na kata ya Nsalala zote za mjini Mbalizi.
“Mkutano huo unalenga kuimarisha chama na kudhihirisha kuwa kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyosema kuwa sisi ni vyama vya msimu si kweli, bali tunao uwezo wa kuimarisha chama kila wakati,’’ alisema Mwangomale.
Alisema chama chake ndicho kinaongoza katika vijiji vya Mbalizi, kata ya Utengule Usongwe na kijiji cha Mshikamano kata ya Nsalala ambako ni mahala panapoonekana kuwa na vuguvugu kubwa la kisiasa na makao makuu ya siasa za wilaya ya Mbeya vijijini.
“Mbali na Lema, wabunge wengine ambao tumewaalika ni Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), na Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa,’’ alisema Mwangomale.
No comments:
Post a Comment