Saturday, July 20, 2013

Tendwa aumbuka

YABAINIKA ALIBARIKI CHADEMA KUANZISHA KIKUNDI CHA KUJIHAMI
LICHA ya kuwapo kwa shutuma mbalimbali zinazopinga mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzisha kikundi cha kujihami cha Red Brigade kitakachotoa ulinzi kwa viongozi wao, imebainika kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa alitoa baraka za kuanzishwa kwake.
Tanzania Daima imeona nakala ya barua ya mwaka 2005 kutoka katika ofisi ya Tendwa, ikionyesha kubariki jambo hilo ambalo katika siku za hivi karibuni limezua gumzo kubwa na kusababisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuhojiwa na polisi kuhusiana na kauli zake.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa Desemba 30, 2004 ofisi ya msajili wa vyama siasa ilimwandikia Katibu Mkuu wa CHADEMA barua yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/29 ikitaka ufafanuzi baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa chama hicho kinataka kuanzisha kikundi cha kujihami (Red Brigade).
“Kulingana na Ibara ya 9 (2) (c) ya Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa 1992, ibara ya 147 na 148 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi, kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kinyume cha sheria hizo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo ambayo Tanzania Daima inayo iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa, inaeleza kuwa kuvunjwa kwa sheria hizo kutasababisha CHADEMA kufutwa.
CHADEMA baada ya kupata barua hiyo, Januari 6 mwaka 2005 iliijibu kuwa kikundi kinachozungumziwa ni walinzi wa ndani ya chama, vijana wa kike na wa kiume, wanachama wa CHADEMA, watu wasio na silaha, chini ya usimamizi wa kurugenzi ya ulinzi na usalama ya chama hicho.
“Kikundi kinachokusudiwa kuundwa ni kutokana na Katiba ya CHADEMA ambayo inaruhusu uundwaji wa Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama chini ya Katiba ya CHADEMA, kifungu cha 7.6.4 (h),” inaeleza barua ya CHADEMA yenye kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/64 iliyosainiwa na Suzan Kiwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Chama hicho kiliilaumu serikali kwa vitisho ilivyotoa vya kutaka kukifuta endapo kingeendelea na kusudio la kuanzisha kikundi hicho.
Hata hivyo, baada ya ufafanuzi huo, Januari 11 mwaka 2005, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, ilipopata majibu hayo ya CHADEMA, ilieleza kuwa kwa madhumuni yaliyoelezwa na chama hicho inakubaliana na malengo ya kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama.
“Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwa madhumuni mliyoyatoa kwenye barua yenu C/HQ/ADM/62 inakubaliana na maelezo yenu ya kuanzishwa kwa kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa ndani ya chama ingawa Katiba ya CHADEMA haijatoa ufafanuzi huo, vinginevyo tunawatakia kila la heri kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho,” ilisema barua ya msajili wa vyama vya siasa nchini.
Barua hiyo yenye kumbukumbu Na. RPP/CHADEMA/72/32 iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa nchini, pia iliwatakia kila la heri CHADEMA kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho.
Nakala za majibu ya Ofisi ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar Mapuri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na Siasa, Muhammed Seif Khatib; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu; Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.
CHADEMA waibua mjadala
Julai 9 mwaka huu akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya CHADEMA mbele ya vyombo vya habari, Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe alitangaza mpango wa kuboresha vikundi vya mafunzo ya kujilinda.
Baada ya kauli hiyo watu mbalimbali akiwemo Rais Jakaya Kikwete, walijitokeza kuupinga mpango huo kwa madai kuwa utasababisha uvunjivu wa amani na utulivu vilivyodumu kwa muda mrefu hivi sasa.
Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa pia alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CHADEMA yenye kumbukumbu Na. 112/123/16A/3 kukitaka chama hicho kuacha kutekeleza mpango huo kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi ikiwamo sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 hali inayoonyesha kujikanganya kwa ofisi hiyo kwani awali ilisharuhusu kitu hicho.
Barua hiyo kutoka ofisi ya msajili inaongeza kuwa; “Kifungu cha 9(2) (c) cha sheria ya vyama vya siasa kinakataza chama cha siasa kuruhusu kutumika, kushabikia au kutumia nguvu na vurugu ili kufikia malengo yake ya kisiasa.”
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na Sisty L. Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, madai ya CHADEMA kusema kuwa “Chama Cha Mapinduzi (CCM) wana kambi za mafunzo ya kupambana   isiwe kisingizio cha vyama vingine vya siasa kuvunja sheria ya vyama vya siasa.”
Msajili pia kupitia barua hiyo amesema “kama CCM wanakiuka sheria, ni jukumu la CHADEMA, kila chama na kila Mtanzania kutoa taarifa na ikiwezekana na ushahidi katika taasisi husika ikiwamo ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ili suala hili lishughulikiwe kisheria.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa katika majibu yake aliifahamisha Ofisi ya Msajili kuwa matumizi ya nguvu ikiwamo silaha kwa ajili ya ulinzi wa maisha au mali yameruhusiwa na sheria ya jinai kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria ya Tanzania.
“Nimeshangazwa sana na kauli yako kwamba vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa vinapaswa kuwa na wanachama wasiokuwa na mafunzo ya kijeshi au ukakamavu kama ilivyo kwa walinzi wa majumbani, kauli hii inadhihirisha ufahamu wako mdogo wa mambo haya. Kwanza walinzi wa majumbani na maofisini wanaoajiriwa na utitiri wa kampuni binafsi za ulinzi zilizosajiliwa nchini kwetu hupatiwa mafunzo ya ulinzi na ukakamavu na wengine hupatiwa silaha za moto,” alisema Slaa.
Alisema kauli hiyo ya msajili wa vyama vya siasa kwamba jukumu la vikundi vya ulinzi si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru, ni hatari sana kwani inawapotosha wananchi wasitumie haki yao ya kujilinda wanaposhambuliwa au kudhuriwa na wahalifu wa kisiasa.
“Barua yako inatutishia kwamba endapo tutatekeleza mpango wetu wa mafunzo kwa kikundi chetu cha ulinzi utakuwa si uamuzi wa busara kwa uhai wa chama chetu.
“Kwa maneno mengine endapo tutatekeleza haki yetu ya kujilinda kama tunavyoruhusiwa na sheria za nchi yetu, kama tulivyoeleza katika barua hii, utatumia mamlaka yako kumaliza uhai wetu kama chama cha siasa kwa kufuta usajili. Hatutaki kuamini kwamba na wewe pia unatumiwa na CCM kukandamiza na kutoa vitisho kwa chama kingine kwa manufaa yake,” alisema Dk. Slaa.

No comments:

Post a Comment