CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kamwe hakitakabidhi ushahidi wake kwa Jeshi la Polisi nchini, hadi Rais Jakaya Kikwete atakapounda tume ya kijaji. Kauli hiyo, imetolewa mjini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe baada ya kutoka kuhojiwa makao makuu ya polisi.
“Msimamo wa chama chetu, ni kwamba hatutatoa ushahidi polisi hadi Rais Kikwete atakapounda tume ya kijaji, hii ndo kauli kubwa niliyowaambia polisi leo (jana),
“Nimewaaleza tukiwa kama chama tulishamwandikia barua Rais Kikwete ya kuunda tume ya kijaji ya kimahakama na yeye bado hajajibu kama amekubali au laa,
“Sisi tutaendelea kusubiri kauli ya Rais kama ataunda leo hata kesho,tupo tayari kupeleka ushahidi tulionao,”alisema Mbowe.
Alisema baada ya kauli hiyo, maofisa wa polisi wakita CHADEMA kupeleka ushahidi wao kwa maandishi.
“Polisi wametuomba, tuweke uamuzi wetu kwenye maandishi na tuyawasilishe siku ya Ijumaa, wakili wangu Peter Kibatala ameahidi kufanya hivyo,”alisema Mbowe.
Alisema mambo mengi yaliyojadiliana na polisi, ni ya kisheria zaidi, hiyo wakili Kibatala atayaweka kwenye mtiririko na kuyawasilisha.
KUJISALIMISHA
Julai 15, mwaka huu Mbowe alijisalimisha polisi saa 8.00 mchana na kuhojiwa na kikosi maalumu cha makachero wa jeshi hilo.
Hatua ya Mbowe kujisalimisha, ilitokana na tarifa kuwa polisi kuvamia nyumbani kwake saa 6.00 usiku Julai 14, mwaka huu kwa lengo la kumkamata.
Chanzo cha kuaminika kutoka makao makuu ya polisi, kilisema Mbowe alihojiwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za uchochezi anaoufanya kwa kujenga chuki kati ya wananchi na polisi.
Tuhuma nyingine, ni kauli yake aliyowahi kuitoa kuwa polisi inahusika katika tukio la mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15, mwaka huu CHADEMA walipokuwa wakihitimisha mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo kwenye viwanja vya Soweto mjini Arusha.
Katika tukio hilo,watu wanne walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya katika tukio hilo.
Katika tukio hilo,Mbowe alidai Chadema kina ushahidi wa kutosha kuwa polisi wanahusika na tukio hilo kutokana na kuwa na mkanda wa video unaoonyesha tukio zima.
Tuhuma nyingine, ni kwamba Mbowe juu ya kauli yake kuwa kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutohudhuria mazishi ya watu waliofariki dunia katika mlipuko huo,kilihusishwa moja kwa moja kuwa ni ishara ya jeshi hilo kuhusika katika mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment