UAMUZI wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukataa kuwasilisha ushahidi wa mauji ya mlipuko wa bomu uliotokea jijini Arusha, umeliweka njia panda Jeshi la Polisi na hivyo kushindwa kuchukua hatua.
Licha ya jeshi hilo kumhoji Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na kumtaka awasilishe ushahidi huo, kiongozi huyo amekataa agizo hilo akisema kuwa wamekubaliana kuutoa ushahidi huo kwa tume huru ya majaji endapo Rais Jakaya Kikwete ataiunda kama walivyomuomba.
Chanzo chetu ndani ya jeshi hilo, kimedokeza kuwa msimamo huo wa CHADEMA umeliweka njia panda na hivyo kushindwa kuchukua hatua za kuwabaini watuhumiwa wa tukio hilo na kuwafungulia mashtaka kutokana na mkanganyiko wa taarifa zinazotolewa.
Jeshi hilo linadaiwa kuwa awali lilitaka kujiegemeza kwenye kauli za kisiasa za baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali ili kuonyesha kuwa CHADEMA ilisababisha mlipuko huo yenyewe kwa ajili ya kuwahadaa wafuasi na kujitafutia umaarufu.
Hata hivyo, mbinu hiyo ya kutaka kuwasakama baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA inadaiwa kufifishwa na tamko la Mbowe pamoja na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwamba chama kina ushahidi unaoonyesha kuwa tukio hilo lilifanywa na polisi.
“Hapa kuna mkanganyiko hasa baada ya Mbowe kudai wanao ushahidi wa video ya tukio hilo. Wakubwa wetu wamegawanyika na kujikuta wakitoa kauli za kukinzana maana wanahofia wakiwafungulia kesi watu wengine mashtaka halafu CHADEMA ikaonyesha ushahidi tofauti itakuwa ni aibu,” kilisema chanzo chetu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, jeshi hilo mkoani Arusha lilikuwa limewakamata watu wawili raia wa kigeni likiwatuhumu kuhusika na mlipuko huo lakini baada ya Mbowe kugoma kupeleka ushahidi huo, watuhumiwa hao hawakuweza kufunguliwa mashtaka.
Pia katika hali ya kushangaza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa makachero wa Taasisi ya Uchunguzi ya Marekani (FBI) wamefika mkoani Arusha kuchunguza jambo hilo.
Hata hivyo taarifa kutoka ubalozi wa Marekani zilikana FBI kuingia nchini kuchunguza jambo hilo hivyo kusababisha mkanganyiko wa tukio hilo lililovuta hisia kubwa ndani na nje ya nchi.
CHADEMA mara kwa mara imekuwa ikilituhumu jeshi la polisi na makada wa CCM kuendesha harakati za kukidhoofisha kwa kutumia matukio mbalimbali yanayofanywa na chama hicho cha upinzani.
Mmoja wa viongozi wa CHADEMA ameliambia Tanzania Daima, kuwa polisi walikuwa wamepanga kuwatumia FBI kuuhabarisha umma kuwa CHADEMA ilihusika na ulipuaji huo bomu lakini kutokana na mazingira yaliyopo wameshindwa kutekeleza uovu huo.
“Unajua hila za polisi na CCM kila siku zinabadilika lakini kwa bahati mbaya hawajui kuwa wananchi wanajua kinachofanyika, kuna askari hawaridhiki na uovu unaofanywa na wenzao,” alisema kiongozi huyo.
Tanzania Daima, iliwasiliana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, kuhusu sakata hilo ambapo alikataa kulizungumzia akidai msemaji wa jeshi hilo Advera Senso anayo majibu.
Hata hivyo Senso hakuwa tayari kulizungumzia akisema kuwa alikuwa eneo baya na akitoka eneo hilo angelijulisha gazeti hili lakini mpaka tunakwenda mitamboni hakutimiza ahadi hiyo.
Mlipuko huo ambao ulisababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa, ulitokea Juni 15 mwaka huu wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani jijini humo, zikiwa zimepita dakika chache baada ya Mbowe kumaliza kuhutubia na kutelemka katika jukwaa lililokokuwa limeelekezwa bomu hilo.
Siku moja baada ya tukio hilo, serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ilitoa taarifa tata bungeni ikionyesha kulikingia kifua jeshi la polisi na kuwatwisha lawama viongozi wa CHADEMA.
Lukuvi alisema kuwa mkutano wa CHADEMA ulikuwa na ulinzi wa polisi wenye magari mawili waliosimama upande wa kaskazini ya uwanja na mrushaji wa mlipuko huo akiwa upande wa mashariki ya uwanja huo na kurusha kuelekea magharibi.
“Jaribio la askari kutaka kumfuata aliyerusha mlipuko huo zilizuiliwa na makundi ya wananchi ambao walianza kuwashambulia askari kwa mawe na kuwazomea na hivyo polisi kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka mhalifu huyo.
“Hivi karibuni zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki ya raia dhidi ya vijana wetu wa polisi, kuwafanya raia wawachukie, wasiwaamini, wasiwape ushirikiano na kuifanya nchi isitawalike,” alisema Lukuvi.
Aliliongeza kuwa kufanikiwa kutoroka kwa mhalifu wa tukio hilo ni matokeo ya uchochezi unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wanasiasa dhidi ya serikali na polisi na hivyo kuwafanya wananchi wajenge chuki dhidi ya polisi.
Siku chache baadaye viongozi wa CCM pamoja na baadhi ya mawaziri kana kwamba wanafahamu mlipuaji wa bomu hilo, waliitwisha lawama CHADEMA wakidai ilihusika na tukio hilo ingawa hadi leo hakuna aliyehojiwa na polisi kati yao kuthibitisha tuhuma hizo badala yake Mbowe pekee ndiye anaandamwa awapelekee ushahidi.
Makada hao ni Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, ambao walidai kuwa CHADEMA ndiyo imekuwa ikihusika na vurugu zote zinazohusisha mauaji nchini.
Kauli za viongozi hao zilitplewa baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kudai kuwa wanao ushahidi wa kutosha kuwa CHADEMA iliandaa na kuratibu shambulio hilo.
“Ni lazima tuwaze na kuvuka mipaka, kuna mambo ambayo yanawezekana kabisa yakawa yamejificha pale. Watu wanaangalia, wanaojitoa ufahamu wanafikiria CCM inaweza kushiriki.
“Mimi niwaambie CCM hata bila kushiriki ni moja kwa moja inawekwa kwenye lawama jambo kama hilo likitokea. Ila CCM haina ushiriki katika jambo kama hili kwa sababu ndio watu wake kupitia serikali yake wanatakiwa kuwahakikishia usalama,” alisema.
Mwigulu ambaye pia ni mbunge wa Iramba Magharibi aliongeza kuwa hata video ya mauji ya Arusha iliyowekwa kwenye mtando wa You tube inaonesha wazi kuwa yalipangwa.
“Yule aliyekuwa anachukua video eti hakushtushwa kabisa na lile bomu, aliendelea kufuatilia kama vile ni mkanda wa harusi. Iliwahi kutokea wapi mchukua video kwenye mkutano wa hadhara kitu ambacho hakikupangwa kimelipuka, kinaua watu, yeye anendelea kama anachukua send off?” alihoji.
Ghasia naye alidai kuwa CHADEMA wamechochea vurugu Mtwara, Mwanza, Mbeya, Morogoro na sasa Arusha ili maeneo hayo yasipate maendeleo.
Kutokana na mlipuko huo, CHADEMA ilitangaza kuanza mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana wake kwa ajili ya kulinda mikutano na viongozi wake lakini CCM, polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, walikionya chama hicho wakidai kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria za nchi, Katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
Hata hivyo hoja zao zilipingwa vikali na baadhi ya wadau wa siasa na wananchi wakihoji walikuwa wapi kwa kutoionya CCM ambayo ina kikundi cha vijana cha Green Guard ambacho kinapewa mafunzo ya kijeshi na matumizi ya silaha za moto.
Julai 17 mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, alimwandikia Mbowe barua na kumwamuru awasilishe ushahidi wa video aliyodai kuwa nayo ikiwaonesha baadhi yao walivyoshiriki kwenye tukio la mlipuko wa bomu Arusha kabla ya Julai 23 mchana saa nane.
Katika hatua ya kuchanganyana, jeshi hilo Juni 20 mwaka huu, kupitia kwa Mkuu wa Mafunzo na Operesheni, Paul Chagonja, aliwaeleza wanahabari kuwa Mbowe anapaswa kuwa mkweli na kuacha kuuchezea umma kwa alichowaeleza polisi ni tofauti kwani hana ushahidi huo.
Lakini katika hatua ya kushangaza Chagonja huyo huyo ndiye amemwamuru Mbowe kupeleka tena ushahidi huo polisi akitamba kuwa baada ya kukaidi kufanya hivyo, polisi inao makachero wake wanaojua jinsi gani ya kuendelea na kazi hiyo.
Pamoja na polisi kudai Mbowe hana ushahidi, Julai 10 mwaka huu usiku wa manane askari kadhaa wakiwa na silaha walifika nyumbani kwake wamkisaka bila mafanikio wakitaka awapatie video hiyo.
Hata hivyo, kesho yake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alidai hana taarifa za askari wake kufika nyumbani kwa Mbowe.
Muda aliopewa Mbowe umemalizika bila kuwasilisha ushahidi huo, akidai kuwa hawezi kwenda kinyume na msimamo wa chama kwani jeshi hilo ni watuhumiwa kwenye tukio hilo la Arusha.
Juzi jeshi hilo lilimtaka Mbowe kuwasilisha msimamo huo wa utetezi wake kwa maandishi leo ambapo kiongozi huyo wa upinzani alisema mwanasheria wa chama hicho ataandaa maelezo hayo.
No comments:
Post a Comment