Thursday, July 25, 2013

Chadema Kujadili rasimu ya Katiba hadharani

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepanga kuzunguka nchi nzima, kikitumia usafiri wa anga, majini na nchi kavu, kufanya mikutano ya hadhara ambayo itakuwa ni mabaraza yake ya wananchi watajadili rasimu ya katiba mpya na kutoa maoni yao hadharani.

Kimesema kuwa tangu kilipoanzisha agenda ya katiba mpya, kimekuwa na dhamira ya kuona Watanzania wakijipatia katiba inayotokana na matakwa yao, hakitafanya mikutano ya ndani au ya siri kama wanavyofanya wapinzani wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Stendi ya Malori, Majengo, mjini Songea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema utaratibu mzima wa namna mabaraza ya katiba ya chama hicho yatakavyoendeshwa utatolewa hivi karibuni, akisisitiza wanataka katiba mpya inayotokana na mwafaka wa Watanzania wote.

"Tunavyozungumza hapa tayari mabaraza ya katiba yameanza kukutana, lakini kama mnavyojua pia asilimia kubwa yametawaliwa na CCM...lakini sisi pia na Watanzania wengine wote wanaoipenda nchi yao, tunayo fursa ya kuunda baraza letu, tutakuwa na mabaraza ya katiba nchi nzima, ambayo tutayafanya kwenye mikutano ya wazi ya hadhara."

No comments:

Post a Comment