MIONGONI mwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaosisimua watu wanapochangia hoja bungeni ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CHADEMA, Leticia Nyerere. Mwandishi wa Tanzania Daima Jumapili, George Maziku, amefanya mahojiano maalumu na mbunge huyo.
Tanzania Daima Jumapili: Kwa kipindi kifupi ulichokaa bungeni umeonyesha uwezo mkubwa, umekuwa mbunge unayejiamini tofauti na wabunge wengi wanawake, umewezaje kuwa hivyo?
Leticia: Kwanza mimi nimezaliwa na kukulia katika familia ya mwanasiasa, baba yangu marehemu Musobi Mageni alikuwa waziri wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na baadaye akawa Mwenyekiti wa taifa wa CUF.
Kwa hiyo nilijifunza mambo mengi kutoka kwa marehemu baba yangu. Pia nimebahatika kuishi karibu sana na mwanasiasa mahiri, hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere nilipoolewa katika familia yake na nilijifunza mengi kutoka kwake.
Hata hivyo, ujasiri na kujiamini nimeupata kutokana na kuishi kwangu kwa muda mrefu nchini Marekani, ambako jamii ya kule inaheshimu na kuthamini haki za binadamu zikiwamo haki za wanawake.
Wenzetu hawana tofauti kati ya mwanamke na mwanamume, ukiacha tofauti za maumbile tu. Wanaamini kuwa mwanamke na mwanamume wana uwezo sawa wa akili, mawazo na fikra.
Mimi huwa simuogopi mwanamume yeyote kwasababu siamini kama mwanamume ana akili nyingi au uwezo mkubwa wa utendaji kazi kuliko mwanamke, naamini wote tuko sawa na inawezekana mimi mwanamke nikawa na akili na uwezo mkubwa zaidi kuliko mwanamume.
Kwahiyo, kama kuna mwanamume anadhani anaweza kutumia jinsia yangu kama nyenzo ya kupambana nami kisiasa anajidanganya sana.
Akitokea mwamume wa aina hiyo siwezi kulalamika wala kulialia ila nitapambana naye kikamilifu mpaka aione dunia chungu. Mimi namuogopa Mungu pekee, lakini si binadamu kama mimi.
Bonyeza Read More Kuendelea
Tanzania Daima Jumapili: Mwaka 2010 uligombea ubunge katika Jimbo la Kwimba, pamoja na kwamba ilikuwa mara yako ya kwanza lakini ulionekana kuwa na uelewa wa mambo ya siasa na ulitoa upinzani mkubwa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM ambaye ndiye mbunge wa sasa wa jimbo hilo, hali hiyo ilitokana na nini? Je, utagombea tena mwaka 2015?
Leticia: Uelewa na uzoefu wa mambo ya siasa nimeupata Marekani kwasababu mwaka 2008 nilikuwa katika timu ya kampeni ya Rais Barack Obama na nilikuwa kiongozi wa kundi la watu 80 tuliokuwa tukimfanyia kampeni Rais Obama katika Jimbo la Virginia.
Tulipatiwa mafunzo mazuri ya kutuwezesha kusimama majukwaani na kujenga hoja za kutaka Rais Obama achaguliwe, hiyo ilinisaidia sana.
Kuhusu kugombea mwaka 2015, hilo lipo wazi kabisa, najiandaa kugombea tena na ninaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi wa Kwimba.
Tanzania Daima Jumapili: Umezaliwa na kukulia kwenye familia ya mwanachama na kiongozi wa TANU na baadaye CCM, baadaye ukaolewa kwenye familia ya mwasisi wa TANU na CCM hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere; ilikuwaje wewe ukajiunga na chama cha upinzani?
Leticia: Itikadi haina uhusiano wowote na mahusiano ya kifamilia. Itikadi ni mtazamo binafsi wa mtu na inatokana na uchambuzi wa kina anaoufanya kila mtu kuhusu mambo mbalimbali, iwe siasa, uchumi au jamii.
Mimi siamini kwamba mtazamo wa baba au mama kuhusu siasa unapaswa kuwa pia mtazamo wa watoto, kila mtu ana uhuru wake wa kuamini chochote bila kuingiliwa na wazazi au wanafamilia wengine.
Kwa mfano, kule Marekani aliyekuwa Gavana wa California, Anold Schwazniger, ni mwanachama wa Chama cha Republican wakati mkewe ni mwanachama wa Democratic na hapakuwa na tatizo lolote.
Hata baba mkwe wangu hayati Mwalimu Nyerere nilikuwa nikimwambia wakati wa uhai wake kuwa mfumo wa chama kimoja cha siasa haufai.
Napenda ifahamike kuwa haifai na ni kinyume cha demokrasia na haki za binadamu kwa mzazi, mume au mke kuwalazimisha wanafamilia wao kufuata itikadi zao. Tunapaswa kubadilika haraka kimtazamo ili kila mtu afurahie uhuru wake wa kisiasa.
Tanzania Daima Jumapili: Kuna watu wanadai kuwa viti maalumu haviwasaidii wanawake kujenga ujasiri na uwezo wa kisiasa na badala yake wanadai vinawapumbaza na wanataka vifutwe, wewe unasemaje?
Leticia: Nafikiri ni muhimu viendelee kuwapo kwa sababu ni muhimu wanawake kujumuishwa kwa usawa katika vyombo vya maamuzi na kutunga sera katika nchi.
Wanawake ni kundi kubwa sana na wana mchango mkubwa sana katika kila nyanja ya maisha ya binadamu, iwe uchumi, siasa, au jamii, hivyo wanastahili kuwakilishwa kwa usawa na wanaume.
Kwahiyo, cha kujadili hapa kwa mtazamo wangu ni namna ya kuwapata hao wawakilishi wa wanawake katika vyombo hivyo vya kutunga sheria na sera, na mimi ninaunga mkono mfumo uliopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba kwamba kuwe na wagombea wawili katika kila jimbo, yaani mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.
Tanzania Daima Jumapili: Watu wanadai kuwa wabunge wanawake wengi hawana msaada kwa wanawake wenzao walio nje ya Bunge, na kwamba wengine wamekuwa wakiwahujumu wanawake wenzao wanaoonyesha kunyemelea nafasi zao, una maoni gani kuhusu hilo?
Leticia: Sijui kwa wabunge wengine, lakini kwa upande wangu siamini kama kuna ukweli wowote kwasababu nimekuwa nikiwasaidia wanawake wengine hususan katika Jimbo langu la Kwimba kuwajengea uwezo wa kisiasa na kiuongozi.
Pia ni wajibu na jukumu la kila mwanamke kuonyesha utayari wa kuwa mwanasiasa. Lazima wewe binafsi ufanye kazi kwa bidii na ujiandae kikamilifu kwa kila nyanja ili kukuwezesha kuwa mwanasiasa na kiongozi katika jamii yako, usisubiri kuwezeshwa na mtu, mimi nilifanya hivyo mpaka kufikia hapa nilipo.
Tanzania Daima Jumapili: Kuna maneno ya hapa na pale kwamba ninyi wabunge wanawake wengi wenu mmepata nafasi hizo kwa upendeleo wa undugu, urafiki na hata rushwa ya ngono, na kwamba wengi wenu hamna uwezo, nini maoni yako kuhusu tuhuma hizi?
Leticia: Si kweli kabisa na ni dharau mbaya sana kwa wanawake wote. Kila chama kina njia na vigezo tofauti vya kuwapata wabunge wanawake. Sisi katika CHADEMA tuna vigezo vyetu ambavyo vilitumiwa kuwapata wabunge wanawake wote wa chama chetu, hapakuwa na upendeleo wa aina yoyote.
Kwa mfano, mimi sikujua hata kidogo kuwa nitakuwa mbunge kwasababu wakati wa mchakato nilikuwa kwenye kampeni zangu za ubunge Jimbo la Kwimba. Na baada ya uchaguzi nilianza kuwasiliana na mwajiri wangu nchini Marekani kumuomba nirejee kazini kwa sababu nilikuwa nimeshindwa kuchaguliwa mbunge. Baadaye Tume ya Uchaguzi ilitangaza majina ya wabunge wa viti maalumu na jina langu likawemo, ndipo nikaahirisha kurudi Marekani.
Tanzania Daima Jumapili: Wewe ni mwanamke mwenye familia, unafanyaje kutofautisha majukumu yako ya kikazi na kifamilia?
Leticia: Sipati shida, nina muda wa kufanya kazi zangu kama mama wa familia na pia muda wa kutekeleza kazi zangu kama mbunge na mwanasiasa.
Familia yangu inaelewa kuwa nina wajibu wa kufanya kazi na wakati mwingine kusafiri kikazi, hawana tatizo. Isitoshe sina watoto wadogo nyumbani, watoto wangu wote ni wakubwa na wapo Marekani wanasoma vyuoni.
Tanzania Daima Jumapili: Wewe ulikuwa waziri kivuli, ilikuwaje ukajiuzulu?
Leticia: Nilitaka kuwapatia watu wengine nafasi ya kujifunza, hapakuwa na tatizo lolote kati yangu na viongozi wangu ndani ya Bunge wala katika chama. Ni vizuri kila mbunge wa CHADEMA akapata nafasi ya kujifunza mambo ya uongozi.
Tanzania Daima Jumapili: Unafanya nini kama haupo bungeni? Je, unasoma au unafanya biashara?
Leticia: Nasoma shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT). Nasoma sayansi ya siasa na sasa hivi nafanya utafiti na nimeamua kutafiti masuala ya wanawake na uchaguzi Tanzania, na nategemea kumaliza mwakani.
No comments:
Post a Comment