KATIBU Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Deogratias Munishi, amesema kuwa serikali ya CCM imekosa maarifa ya kutambua kuwa elimu bora inayokidhi mahitaji ya taifa ndiyo njia ya kutatua tatizo la ajira nchini.
Munishi alisema fursa za ajira zimejaa duniani kote, wanaozifaidi ni wale wenye maarifa na ujuzi ambao msingi wake mkuu unatokana na elimu bora wanayoipata.
Alisema anashangaa kuona serikali ya CCM imefilisika kifikra na maono ya kulinasua taifa kutoka kwenye janga hili, kwa kushindwa kuifanya sekta ya elimu kutokuwa kipaumbele kwenye bajeti yake ya mwaka mpya wa fedha na hata bajeti zilizopita.
Alisema kuwa serikali ya CCM imeendelea kuwaweka vijana wa taifa hili rehani kwa kuendelea kuua viwanda ambavyo kimsingi ni injini nyingine ya kutatua tatizo la ajira nchini.
“Viwanda ndiyo sekta inayoweza kuajiri watu wa aina yoyote, wenye ujuzi na wasio na ujuzi, wenye elimu na wasio na elimu, lakini serikali ya CCM imeshindwa kulitambua hili,” alisema.
Alisema, taifa linahitaji uongozi wenye maono mapya ili kujenga taifa bora.
No comments:
Post a Comment