BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina wabunge wengi kutoka vyama mbalimbali vya siasa. Kwahiyo, kutokana na idadi kubwa ya wabunge, mbunge anapaswa kufanya kazi kubwa kuweza kujipambanua na kuonyesha uwezo, umakini na uchapa kazi wake.
Christine Lissu, mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ni mmoja wa wabunge wachache katika Bunge hilo aliyefanikiwa kujipambanua kwa kuonyesha uwezo mkubwa katika kutekeleza wajibu wake ndani na nje ya Bunge. Gazeti hili lilifanikiwa kufanya mahojiano na mbunge huyo machachali na hapa anaeleza jinsi alivyoingia katika siasa.
Tanzania Daima Jumapili: Wasomaji wetu wangependa kujua ilikuwaje ukaingia katika siasa za upinzani?
Lissu: Kaka yangu Tundu Lissu ndiye aliyenivutia kuingia kwenye siasa hususan kujiunga na CHADEMA. Nilikuwa navutiwa sana na harakati zake za kutetea haki za wananchi wanyonge na kupinga ukandamizaji, nikaamua kujiunga na CHADEMA ili kumuunga mkono.
Halafu unajua mimi na Tundu tunafuatana kuzaliwa, hivyo tunapendana na kuelewana zaidi. Jambo hilo pia lilisaidia sana kunifanya niungane naye katika harakati zake za kutetea haki za binadamu na kupigania mageuzi ya kisiasa nchini.
Kingine kilichonishawishi kujiunga CHADEMA ni itikadi na sera za chama za kutetea masilahi ya wananchi wanyonge. Hiki ndicho chama pekee nchini ambacho ni tumaini la watu maskini na wanyonge. CHADEMA ndiyo mkombozi wa Watanzania hivyo wanapaswa kukiunga mkono kwa nguvu zote.
Tanzania Daima Jumapili: Tunajua kuwa ndani ya familia yenu wamo wanachama wa chama tawala-CCM, vipi kuna upendo na maelewano kweli katika familia?
Lissu: Ni kweli kabla ya kifo cha baba yetu kulikuwa na Wana CCM wawili, yaani marehemu baba na kaka yetu wa Arusha, Alute Mughwai Lissu, kwa sasa amebaki Alute peke yake. Hata hivyo, hakuna tofauti yoyote kati yetu, tunapendana na kuheshimiana sana, kwa sababu hivyo ndivyo tulivyolelewa na wazazi wetu.
Unajua Tundu alifanikiwa kutubadilisha karibu familia nzima, hata marehemu mama yetu alikuwa mwanachama wa CHADEMA na alikuwa akihudhuria mikutano yote ya Tundu, kwa kweli alikuwa akitutia nguvu sana.
Tanzania Daima Jumapili: Kuna tuhuma kwamba wewe na wabunge wengine wa viti maalumu wa CHADEMA mmepata nafasi hizo kutokana na undugu au uhusiano mwingine na viongozi wa CHADEMA, je, wewe uliteuliwa kutokana na undugu wako na Tundu?
Lissu: Siyo kweli hata kidogo. Wanawake wote wa CHADEMA wana fursa sawa kuomba nafasi za ubunge wa viti maalumu na kuna utaratibu na vigezo vya kutimiza kwa wanawake wote wanaoomba nafasi hizo.
Kwahiyo, wanawake wote tuliopata nafasi hizi tumekidhi vigezo vya chama chetu. Isitoshe mimi nilikuwa mtu wa 20 katika orodha ya chama chetu iliyopelekwa Tume ya Uchaguzi, kama ni upendeleo basi ningewekwa nafasi za juu ili iwe rahisi kupata ubunge kama chama chetu kingepata nafasi chache. Nani alijua kuwa tungepata viti 25 vya wanawake uchaguzi wa 2010?
Tanzania Daima Jumapili: Kuna watu wanasema viti maalumu haviwasaidii wanawake kuwajengea uwezo wa kisiasa na kiuongozi, wewe una maoni gani?
Lissu: Siyo kweli. Viti maalumu vinasaidia sana kuwaandaa wanawake kuwa wanasiasa na viongozi mahiri. Kwa wanawake wenye malengo ya kufika mbali kisiasa na kiuongozi, viti maalumu vinasaidia sana kuwapa ujasiri na uzoefu wa uongozi, hivyo ni vizuri viendelee kuwapo kwasababu mfumo dume bado una nguvu katika jamii yetu.
Hata hivyo, napendekeza yafanyike mabadiliko ya mfumo wa kuwapata ili kuondoa masimango yanayojitokeza kutoka kwa baadhi ya wananchi wanaofikiri kunakubebwa au kupendelewa na kwamba hatuna uwezo.
Tuanzishe mfumo mpya, ambao utawawezesha wanawake kupigiwa kura. Tunaweza kuchukua mfumo wa kusimamisha wagombea wawili katika kila jimbo moja, mmoja akiwa mwanamume na mwingine mwanamke au kuwe na mfumo wa uwiano.
Bonyeza Read More Kuendelea
Tanzania Daima Jumapili: Unazungumziaje mtazamo wa jamii kuhusu wanasiasa au viongozi wanawake? Je, tupo tayari kuwa na rais mwanamke?
Lissu: Mtazamo hasi dhidi ya wanawake umeanza kupungua, jamii sasa imeanza kutuelewa na kutukubali kuwa tunaweza.
Mimi naamini Tanzania tupo tayari kuwa na rais mwanamke, kwa sababu kuna wanawake wengi sana wameonyesha uwezo na umakini mkubwa katika uongozi. Nina uhakika Watanzania hawatasita kumchagua rais mwanamke kama itatokea akaomba nafasi hiyo hususan kupitia CHADEMA.
Tanzania Daima Jumapili: Kwa ninyi wanawake wachache mliobahatika kuingia katika vyombo vya maamuzi kama Bunge, mnawasaidiaje wanawake wenzenu wanaotaka kuwa wanasiasa na viongozi?
Lissu: Sisi katika chama chetu tunao utaratibu wa kuwasaidia na kuwawezesha wenzetu waliopo nje ya uongozi kwa kuwajengea uwezo na ujasiri wa kuthubutu kuomba uongozi wa ngazi yoyote.
Tunafanya mikutano, semina na makongamano ya kujengeana uwezo. Tunawahimiza wanawake wenzetu kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani na nje ya chama.
Tanzania Daima Jumapili: Vipi, utagombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2015?
Lissu: Nitagombea, nimejipanga kugombea katika jimbo moja la Mkoa wa Singida kama hayajafanyika mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Siwezi kusema kwa sasa jimbo nitakalogombea kwa sababu ni mapema mno, inaweza kuharibu mikakati yangu ya ushindi lakini itakuwa Mkoa wa Singida.
Tanzania Daima Jumapili: Singida ni mkoa mgumu sana kupokea mabadiliko ya kisiasa, vipi hali ya uhai wa CHADEMA kimkoa?
Lissu: Tundu Lissu amefanya kazi kubwa kuibadili Singida. Watu wengi wamehamasika kupenda mageuzi. Kwa sasa kuna mwamko mkubwa sana kwa karibu mkoa mzima wanataka mabadiliko.
Tanzania Daima Jumapili: Chama chenu kinaonekana kuandamwa na kusakamwa sana kwa tuhuma mbalimbali, kwanini inakuwa hivyo?
Lissu: Hao wanaotusakama na kutuzushia tuhuma mbalimbali za uongo ni CCM na wanafanya hivyo kwasababu wanatuogopa, sisi tumeonyesha kuwa ni chama tishio kwa mustakabali wao, hawajiamini, wana hofu ya kushindwa 2015.
Bila shaka chama chetu kipo katika mwelekeo mzuri sana, na nina hakika tutawashinda CCM kwa kishindo mwaka 2015 na kuongoza dola.
Tanzania Daima Jumapili: Ni kiongozi gani wa ndani au nje ambaye umekuwa ukivutiwa naye, na ambaye ungependa uwe kama yeye?
Lissu: Kwanza kabisa kwa kiongozi wa kijamii ningependa kuwa kama mama yangu mpenzi. Mama yangu alikuwa mwanamke na kiongozi wa familia wa kuigwa na ningependa niwe kama yeye kutokana na kumudu kulea familia yake kubwa bila kutetereka.
Pili, kwa kiongozi wa kisiasa ningependa kuwa kama Winnie Mandela. Nampenda sana Winnie kutokana na ujasiri wake. Alimuunga mkono mzee Mandela wakati wote alipokuwa gerezani na alikuwa nembo ya ANC na kiunganishi cha wananchi wote wa Afrika Kusini wakati Mandela akiwa kifungoni, napenda kufikia mafanikio yake.
No comments:
Post a Comment