Sunday, July 21, 2013

CHADEMA yaishambulia CCM

WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Ziwa Magharibi, wameishambulia serikali ya CCM kwa kusema ndiyo iliyoasisi umaskini wa Watanzania kutokana na kuridhia mikataba mibovu dhidi ya rasilimali za taifa.
Kufuatia hayo, wamesema kabla ya Tanzania kupata uhuru wake mwaka 1961, serikali ya kikoloni ilikuwa ikitoza ushuru asilimia 15 kwa makampuni makubwa ya uchimbaji madini, lakini kwa sasa serikali ya CCM inatoza ushuru wa asilimia tatu kwa makampuni hayo.
Aidha, waliituhumu serikali kwa madai kwamba inaongoza nchi bila kufuata utawala bora, kwa kuwa sasa suala la utawala bora halipo na halizingatiwi na viongozi waliopo madarakani.
Kauli hiyo ilitolewa kwa nyakati tofauti, na wabunge hao wakati walipokuwa wakihutubia mikutano ya hadhara katika miji ya Lunzewe, Ushirombo na Kijiji cha Bulega wilayani Bukombe, mkoani Geita, ikiwa ni operesheni maalumu ya ‘Vua Gamba, Vaa Gwanda’.
Wakihutubia mikutano hiyo, Mbunge wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk. Anthony Mbasa pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kagera, Conchesta Rwamlaza, kwa ujumla wao waliishambulia serikali ya CCM kwa kuwatumbukiza Watanzania katika tanuru la umaskini.
Akizungumzia suala la mikataba mibovu, Mbunge wa Bukombe, Profesa Kahigi alisema serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuwanusuru wananchi katika dimbwi la umaskini, ambao unatokana na kuwapo kwa mikataba ya kinyonyaji dhidi ya migodi ya madini.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Bukombe, Profesa Kahigi aliwaomba Watanzania wote kuunganisha nguvu kuiondoa madarakani serikali ya CCM mwaka 2015, na kwamba dira ya CHADEMA ni kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali zilizopo.
Naye, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk. Mbasa, alisema harakati za CHADEMA ni kuhakikisha inawakomboa wananchi, ikiwa ni pamoja na kuwanasua wananchi na tatizo la umaskini unaoonekana kuota mizizi sasa.
Akitolea mfano wa ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama, Dk. Mbasa alisema: “Ujio wa Rais Obama wa Marekani hapa nchini kwetu Tanzania, jumla ya mikataba 17 imesainiwa na viongozi wa serikali bila kuwashirikisha wananchi kuhusu miradi husika.”
Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kagera, Conchesta Rwamlaza, aliwaomba wananchi ngazi zote kushikamana pamoja kuhakikisha wanapigania maendeleo yao kwa kuiondoa CCM madarakani.

No comments:

Post a Comment