KODI YA LAINI YAWACHONGANISHA
NI dhahiri kodi ya sh 1,000 kila mwezi kwa wamiliki wa laini za simu sasa inatishia uhai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimeamua kuisulubu serikali na wabunge wake walioipitisha katika kikao cha Bunge la bajeti kilichomalizika hivi karibuni mkoani Dodoma.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa licha ya CCM kuishutumu serikali kuweka kodi hiyo, makada wake wamesema kilichofanyika kilipata baraka za viongozi wa chama hicho, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la mawaziri.
Baadhi ya makada wa CCM waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa sharti la kufichwa majina yao, wameelezwa kushangazwa kwao na taarifa ya Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuwa chama hicho tawala kinapinga tozo hiyo kwa sababu itaongeza mzigo kwa mwananchi wa kawaida na kusababisha usumbufu usiokuwa na sababu kwa walalahoi.
Walibainisha kuwa kitendo kilichofanywa na CCM kitachochea zaidi hasira za wananchi dhidi ya chama hicho kinachounda serikali inayolalamikiwa kutowajali wananchi, kwa kuamua kuweka tozo kwenye laini za simu badala ya kuwabana zaidi matajiri na wawekezaji wanaokwepa kodi kila kukicha.
Waliongeza kuwa CCM imepima upepo wa wananchi dhidi ya kodi hizo zilizoanza kutumika mwaka huu na kubaini kuwa inajiandalia wakati mgumu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.
Inaelezwa kuwa hofu hiyo imechagizwa zaidi na matokeo ya hivi karibuni kwenye chaguzi ndogo za udiwani, ambapo CHADEMA imeonekana kuimarika zaidi huku CCM ikipoteza viti visivyopungua vitatu.
Wakati CCM wakionekana kuhaha kujinusuru, viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwalaumu wabunge wa chama tawala na wale wachache wa upinzani waliopitisha sheria ya kuruhusu tozo hilo.
Wabunge wa CHADEMA wakati wa mjadala huo walikuwa nje ya Bunge mkoani Arusha kuhudhuria msiba wa watu waliofariki dunia katika mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15, mwaka huu katika viwanja vya Soweto wakati wa ufungaji wa kampeni za udiwani wa chama hicho.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema kuwa hataacha kufanya siasa kwenye suala la tozo za kadi za simu hadi pale kodi hiyo itakapofutwa ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha.
Mnyika alitoa msimamo huo juzi baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, kueleza kuwa mbunge huyo amekuwa akichukua uamuzi huo baada ya kuona malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Mnyika anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea, namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili,” alisema.
CCM hivi sasa imo katika wakati mgumu, kwani kauli aliyoitoa Makamba juzi kwenye mitandao ya kijamii alieleza kuwa wizara yake ilipinga tangu awali mpango huo kabla ya kupitishwa na kuwa sheria na anaamini itaondolewa.
“Sikubaliani na hili suala na kupita kwake ilikuwa ni kuzidiwa nguvu. Lakini najua haliwezi likatekelezeka ni lazima litabadilishwa kwa kuangalia eneo jingine la kutoza kodi,” alisema Makamba.
Kodi hiyo ya tozo ya laini za simu ilizua mjadala mkubwa bungeni baada ya bajeti kutangazwa, kitendo kilichomfanya Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, kuomba serikali ipewe muda wa kutosha wa kujadili suala hilo.
Baada ya majadiliano na Kamati ya Bajeti ambayo inaongozwa na Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM), Waziri Mgimwa pamoja na wabunge waliridhia wananchi waanze kutozwa fedha hizo kuanzia Julai mosi mwaka huu.
Mgimwa aivimbia serikali
Wakati CCM ikitaka serikali kufuta kodi hiyo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Wiiliam Mgimwa, alisema suala hilo halikwepeki na litaanza kufanya kazi kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mgimwa alisema hakuna mabadiliko katika suala hilo na lengo lililokusudiwa litabaki palepale, kutoza tozo hilo.
Waziri huyo alisema kuwa dhumuni la kuanzisha na kukusanya kodi hiyo ni kuiwezesha serikali kuweza kutoa huduma bora za maji, umeme, na barabara hasa katika maeneo ya vijijini.
Dk. Mgimwa alisema wiki hii walikutana na wamiliki wa vyombo vya habari (MOAT) ambao wametoa mapendekezo, mawazo, ushauri na tahadhari kuhusu suala hilo ambapo serikali imechukua mawazo hayo na kwenda kuyafanyia kazi.
Alisema serikali haijiamulii mambo, bali hushirikiana na kufuata mawazo kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya vyanzo na mapendekezo ya kodi.
“Kwa hili la kodi ya laini za simu ni pendekezo lililotoka kwa wabunge kupitia Kamati ya Bunge,” alisema.
Aliongeza kuwa suala la kodi ya laini za simu ni miongoni mwa mapendekezo 67, ambapo serikali imechukua mapendekezo 22 ili kufanyia kazi na imetokana na mapendekezo ya wabunge.
“Kwa sasa hili ni suala la kisheria, kwa kuwa jambo likishapita bungeni linapaswa lifuate mkondo huo huo. Kulibadili ni lazima lipelekwe tena bungeni.
“Hayo yalipendekezwa na Kamati ya Bunge si serikali. Tena walipendekeza vyanzo 67 vya kodi likiwamo hilo la kadi za simu. Walipendekeza tukate sh 1,450 kwa mwezi, lakini sisi serikali tukashusha hadi sh 1,000, yaani kila mwananchi akatwe sh 33.3 kwa siku na mapato yatakayopatikana yatakwenda kuboresha miradi ya maji, umeme vijijini na barabara,” alisema Dk. Mgimwa.
Ujumbe wa kuondoa simu wasambazwa
Wakati huo huo, baadhi ya wamiliki wa simu kuanzia jana majira ya saa 3:00 asubuhi wamekuwa wakipokea ujumbe wa kuhamasishana kuchomoa laini za simu pindi ifikapo Julai 29 hadi 31, mwaka huu.
Aidha, kwa ujumbe ambao gazeti hili linao, ulihamasisha kuchomoa laini za simu katika kipindi hicho ili kugomea kodi hiyo kwa ajili ya kulazimisha mabadiliko ya sheria hiyo.
“Chomoa simu kadi siku zifuatazo kugomea kodi ya sh 1,000 kwa mwezi kuhamia laini nyingine Julai 29 (Vodacom), Julai 30 (Airtel) na Julai 31 (Tigo na laini nyingine), tumia nguvu yako ya fedha kulazimisha mabadiliko ya kisera, tunaweza, sambaza ujumbe huu,” ilisema taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment