Friday, July 5, 2013

CHADEMA yawanasa Lowassa, Mwigulu

WABUNGE WAKE NAO WAMTEGA SPIKA WA BUNGE
MBINU zinazosukwa na vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba ili kukidhohofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Mwanza zimefichuka.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) na Mwigulu wanatajwa kutaka kutumia harambee ya kuchangia wafanyabiashara wadogo (Machinga) eneo la Makoroboi jijini hapa leo ili kufanikisha hujuma zao hizo za kisiasa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Magharibi, Peter Makere, kupitia idara yao ya usalama wamefanikiwa kunasa mikakati hiyo ya kutaka kuwadhoofisha.
Alisema kuna baadhi ya makada wa CCM wamejipanga kuhujumu kadi na baadhi ya vifaa vya uenezi vya CHADEMA kwa ajili ya kuvirudisha kwenye harambee hiyo ili kuhadaa umma kuwa chama hicho hakikubaliki.
Makere alisema kuwa mgeni rasmi wa harambee hiyo, ametajwa kuwa ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Lowassa ambaye ataongozana na makada wengine wa CCM, akiwemo Mwigulu.
“CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, imebaini mbinu chafu na ovu zinazopangwa na makada wa CCM kuhujumu kadi na vifaa vyetu. Hujuma hizi zinaandaliwa ili kuuhadaa umma eti CHADEMA haikubaliki. Vifaa hivi vimepangwa kurudishwa kwenye harambee ya kuchangia machinga itakayoongozwa na Lowassa,” alisema.
Alisema kuwa CHADEMA kama chama makini na chenye dira thabiti ya kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye makucha ya CCM yaliyojaa umasikini, wanaomba umma upuuze hujuma hizo na kuendeleza mapambano ya kuiondoa madarakani 2015.
Aidha, Makere aliwaomba wamachinga na wananchi wa Jiji la Mwanza bila kujali itikadi zao wapokee fedha za CCM na waongeze ujasiri na mbinu za kuiondoa madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema muda huu ni wa msimu, kwani baadhi ya viongozi wa CCM wanaotafuta urais kwa gharama kubwa kupitia makanisa na misikitini, wameanza kujipendekeza ili waungwe mkono, hivyo ni vema Watanzania wakawaogopa watu hao kama ukoma.
“CCM lazima ibadilike, iachane na siasa uchwara, hadaa, ghiliba na mazingaombwe. CHADEMA tunataka chama hicho kupitia viongozi wake kiwaambie Watanzania kimewafanyia nini katika sekta za elimu, afya, maji, ajira kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru,” alisema Makere.




Wabunge wamtega spika
Kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda kushindwa kuahirisha Bunge kama sehemu ya kutoa nafasi kwa wabunge kuomboleza vifo vya wafuasi wa CHADEMA waliolipuliwa kwa bomu jijini Arusha, kimezidisha uhasama baina ya taasisi hiyo na wabunge wa chama hicho, Tanzania Daima limebaini.
Uhasama huo umefikia hatua ya wabunge wa CHADEMA kuazimia kukataa kukatwa fedha zao za posho ya kujikimu ambazo hutolewa kama rambirambi ya Bunge pindi linapotokea tukio kubwa la vifo na majeruhi wakati vikao vya Bunge vikiendelea.
Utamaduni huo umekuwa ukitumiwa na Bunge kwa wabunge kukatwa posho zao za siku moja sh 80,000, jambo ambalo halikufanyika kwa waathirika wa tukio la mlipuko wa bomu jijini Arusha la Juni 15 mwaka huu, kwenye mkutano wa CHADEMA eneo la Soweto, ambako watu wanne walipoteza maisha na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wabunge hao wa CHADEMA waliweka msimamo huo wakiwa jijini Arusha walikoweka kambi wiki nzima kwa ajili ya kuomboleza wafuasi wao waliopoteza maisha na kuwasaidia majeruhi.
Baada ya kupitisha azimio hilo, walimkabidhi jukumu mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ili kuhakikisha anafikisha taarifa hiyo kwa uongozi wa Bunge.
Akithibitisha juu ya azimio hilo jana, Lissu alisema ni kweli waliazimia hivyo, kuwa hawako tayari kukatwa tena fedha zao na uongozi wa Bunge bila ridhaa yao.
“Kama uongozi wa Bunge haukuona msiba wa wafuasi wetu Arusha ni msiba unaowahusu wabunge wote, basi wasituhusishe kwa kuchangisha kwenye misiba wanayoitambua wao,” alisema Lissu.
Mbunge mwingine wa CHADEMA kutoka Kanda ya Ziwa ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa chama, alisema kuwa ni jambo la ajabu kuona wakati wote yanapotokea majanga makubwa ya kitaifa, wabunge wote wamekuwa wakishikamana na kuchangia posho zao bila kujali wanamchangia nani, wa itikadi wala dini gani.
“Wakati Bunge likiendelea, Mtwara kulitokea vurugu mara mbili na Bunge likaahirishwa mara zote mbili. Wabunge tulichangia posho zetu za siku moja kwa waathirika wa matukio hayo bila kujali ni wakina nani. Hata wakati wa mlipuko wa bomu kwenye Kanisa Katoliki eneo la Olasiti jijini Arusha tulifanya hivyo hivyo na Bunge lilituma wawakilishi wake kuwajulia hali waathirika.
“Lakini tunajiuliza ni kwanini lilipotokea tukio la mlipuko kwenye mkutano wetu na wafuasi wetu kupata matatizo, Bunge liliendelea na vikao kama kawaida, Spika wa Bunge wala wabunge wa CCM hakuna aliyetuma rambirambi wala kushiriki mazishi au kupeleka wawakilishi. Utaratibu wetu wa kuchangia posho zetu nao haukufanyia,” alisema.
Aliongeza kuwa ni kwa sababu hiyo wabunge wote wa CHADEMA waliazimia kuachana na utaratibu huo wa kukatwa posho zao kuchangia misiba bila ridhaa yao, kwani Spika wa Bunge na viongozi wenzake wa serikali walikuwa na ajenda yao ya siri katika tukio hilo la Arusha, ndiyo maana waliwabagua wafuasi wa CHADEMA wakiwafanya kana kwamba si Watanzania.
Tangu kutokea kwa tukio hilo, kumekuwa na mvutano mkali baina ya Bunge na CHADEMA hatua iliyowafanya hata wabunge hao kususia kuingia bungeni kuipitisha bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/14.
Akifafanua hatua hiyo ya kususia upitishaji wa bajeti, Lissu alisema kuwa tukio la bomu kwa wafuasi wao halikuwa la bahati mbaya, lakini walijiuliza ni kwanini Bunge halikuahirishwa walau kwa siku moja kama ilivyo utamaduni ili kushiriki kuomboleza msiba huo.
Alisema kuwa pamoja na kwamba kiongozi wao wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai na Godbless Lema wa Arusha Mjini ndio walikuwa wamelengwa kulipuliwa, bado Spika wa Bunge wala Waziri Mkuu hakuna hata mmoja aliyetuma salamu za pole kwa viongozi hao.
“Waliolengwa kulipuliwa ni Mbowe, Lema na James ole Millya, maana hata risasi zilizowaua wale wafuasi wetu wanne zilikuwa zikielekezwa kwa viongozi hao. Sasa tunajiuliza Bunge liliona waliokufa Arusha ni Watanzania, lakini kwa vile walikuwa kwenye mkutano wa CHADEMA haiwahusu, hivyo kama wanajifanya hakuna kilichotokea sisi tungeingia bungeni kufanya nini?” alisema.
Lissu alitaja sababu nyingine kuwa siku zote kila unapotokea msiba mkubwa wa kitaifa wakati Bunge likiendelea na vikao vyake, wamekuwa wakitumwa wawakilishi kuwafariji wafiwa na majeruhi, lakini kwa tukio la Soweto, Bunge halikutuma mwakilishi wake.
Alifafanua kuwa walichukizwa na kitendo cha Spika wa Bunge kupindisha ratiba ya Bunge ili kuwanyima nafasi wabunge wa CHADEMA wasijadili bajeti hiyo, na hivyo kuhoji wangeingia kupitisha kitu gani ambacho hawakushiriki.
“Hatukuweza kuwasilisha maoni ya kambi kutokana na tukio la Arusha, lakini kulingana na ratiba tulimaliza mazishi siku ya Ijumaa tukijua kabisa Jumatatu tungepewa muda wetu wa nusu saa kuwasilisha maoni ya kambi.
“Sio hivyo tu, bali hata wale walioomba kuchangia wangepata nafasi ya kufanya hivyo halafu sasa Jumanne bajeti hiyo ingepitishwa kwa mujibu wa ratiba. Lakini kutokana na hofu kuwa tungejibu mapigo kuhusu madai ya Arusha, waliamua kufanya mbinu za kutunyima nafasi,” alisema.

No comments:

Post a Comment