Namba ya kituo iliyotumika katika mtandao wa simu kutuma ujumbe wa simu unaodaiwa kutoka kwenye namba za Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kwenda kwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ni ya Uingereza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa ingawa uchunguzi unaendelea kumekuwa na ugumu wa kupata taarifa hizo kutoka kwa kampuni ya simu ya Uingereza zitakazoweza kupata ukweli wa mambo.
“Taratibu ndizo zinazoleta ugumu, lakini bado tunaendelea na uchuguzi,” alisema.
Mei 21, mwaka huu, Kamanda Sabas alimsafisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mulongo pale alipowaeleza waandishi wa habari kuwa uchunguzi wa awali kuhusu ujumbe unaodaiwa kutumwa na mkuu huyo wa mkoa umetumwa na mtandao wa simu ya nje.
Ingawa kwa wakati huo alikataa kutaja nchi lakini jana aliitaja Uingereza kuwa ndiko ujumbe huo ulikotumwa.
Katika kipindi cha mwishoni mwa Aprili mwaka huu, vyombo vingi vya habari vikiwamo radio, magazeti na mitandao ya kijamii viliandika na kutangaza habari iliyoelezea shutuma zilizotolewa na Mbunge Lema kuwa aliandikiwa ujumbe wa vitisho kwa njia ya simu na Mkuu wa Mkoa Mulongo ambao ulisomeka:
“Umeruka kihunzi cha kwanza nitakuonyesha mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayoitaka mimi.”
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, ujumbe huo ulidaiwa kutumwa kutoka namba 0752960276 inayotumiwa na Mkuu wa Mkoa Mulongo kwenda kwenye namba 0764150747 inayotumiwa na Lema.
Alisema kufuatia tuhuma hizo, polisi walianza uchunguzi kwa kuzingatia kuwa Mulongo alikanusha kutuma ujumbe wa aina yo yote kwa Lema.
No comments:
Post a Comment