Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakitarudi nyuma katika mpango wa kutoa mafunzo ya ukakamavu kupitia kikundi chake cha red brigade.
Chama hicho kimesema, tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), vyote vikiwa miongoni mwa `vyama vikubwa nchini’, vina vikundi vya aina hiyo.
Mkurugenzi wa Oganizasheni na Mafunzo Chadema, Singo Benson, ametoa msimamo huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Chama hicho kimesema, tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), vyote vikiwa miongoni mwa `vyama vikubwa nchini’, vina vikundi vya aina hiyo.
Mkurugenzi wa Oganizasheni na Mafunzo Chadema, Singo Benson, ametoa msimamo huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Tamko la Chadema kuanzisha mafunzo hayo, limeibua taharuki na kusababisha watu kadhaa akiwamo Rais Jakaya Kikwete, kutaka mpango huo usitishwe.
LENGO LA MAFUNZO
Benson alisema lengo la kuimarisha kikundi hicho, ni kujikinga dhidi ya mashambulizi yanayoelekezwa kwa viongozi, wanachama na wafuasi wake, ambapo CCM ikitajwa kuwa nyuma ya mashambulizi hayo.
Alisema Chadema, imekamilisha maandalizi ya mafunzo yatakayowajumuisha zaidi vijana, ili wapate mbinu za kujikinga na kuwalinda viongozi wao ikiwa ni pamoja na katika mikutano ya hadhara.
Hata hivyo, alisema mpango huo hauhusishi mafunzo ya kijeshi, akidai kwamba mafunzo kama hayo yanatolewa kwa vijana kupitia kambi maalum zinazoratibiwa na CCM.
MAKAMBI YA CCM
Benson alidai kuwa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Igunga mkoani Tabora mwishoni mwa 2011, CCM iliandaa makambi mbalimbali ya kufundisha vijana mbinu za kijeshi.
“Iweje Chadema tuambiwe kuwa ni haramu kwa mwaka huu, wakati mwaka jana vijana wa CCM walifanya mafunzo na paredi ya jeshi ambayo ni hatari kwa nchi,” alihoji.
Alidai kuwa moja ya matokeo ya kambi za vijana wa CCM kule Igunga, ni kupigwa hadi kuuawa kwa Mbwana Masoud na Msafiri Mbwambo waliotokea Arumeru Mashariki.
Alidai kuwa matukio hayo yanajulikana hadi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
AMGEUKIA MWIGULU
Benson alisema IGP Mwema anatakiwa kuanza kuwashughulikia Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba, kwa madai ya kuwa mmoja wa waasisi wa kuwabebesha vijana silaha za kwenda kushambulia raia wasiokuwa na hatia.
Hata hivyo IGP Mwema aliliambia gazeti hili jana kwamba atatoa tamko kuhusiana na sakata hilo Jumatatu ijayo.
“Kikwete (Rais Jakaya Kikwete) awaeleze hao vijana wa CCM wanafanyaje hayo mafunzo yao, na wamekuwa wakitumika kuwapiga viongozi wa Chadema mbele ya polisi na hakuna hatua zinazochukuliwa,” alisema.
Benson alisema kabla ya polisi kuanza kuwashughulikia Chadema, wanapaswa kuanzia CCM.
“Sasa Rais Kikwete aseme hao ni wajasiriamali ama wanajeshi, na kama ni wajasiriamali bunduki walizo nazo ni za nini,” alihoji Benson.
Hata hivyo, alisema kikundi chao walichokianzisha kipo kwa mujibu wa kikatiba na kwamba watafundishwa kulinda haki za Watanzania, kuwalinda viongozi na mikutano ya Chadema.
Alisema mafunzo ya kuimarisha kikundi cha ulinzi cha Chadema yatanza wiki ijayo katika mikoa mbalimbali.
Pia, Benson alisema leo, Chadema wanatarajia kuzindua msimamo wa chama kuhusu rasimu ya Katiba Mpya katika Shule ya Msingi ya Ukombozi iliyopo Manzese jijini Dar es Salaam.
UVCCM NAO WAIBUKA
Kwa upande wake, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), imeshutumu hatua ya Chadema kuanzisha mafunzo kwa kikundi hicho cha ‘Red brigade’.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela, alisema kuwa wana wasiwasi na mafunzo yatakayotolewa na Chadema, yatakuwa na ‘sura ya kigaidi’ kwa vile yatafanyika kwa siri.
“Tunalaani vikali mafunzo hayo, hayana tija yoyote kwa jamii yeyote,” alisema Shigela.
Kwa mujibu wa Shigela, UVCCM haifanyi kazi za ulinzi kama `red brigade’ badala yake wanaangalia ni jinsi gani vijana wanaboreshewa huduma mbalimbali za kijamii kupitia siasa.
WAISEMEA KATIBA MPYA
Shigela aliipongeza rasimu ya Katiba Mpya kupitia Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, kwa kuwaandaa wabunge wenye umri mdogo, tofauti na ilivyokuwa awali.
“Rasimu ya Katiba Mpya inaainisha kwamba wagombea nafasi za ubunge wanatakiwa kuwa na umri wa miaka 21 hadi 25,ila awe anakidhi kiwango na sifa za ubunge, hili ni jambo jema”, alisema.
No comments:
Post a Comment