Friday, July 26, 2013

Warioba ‘amnanga’ aliyetoa maoni kwa waraka wa CCM

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amewakosoa wajumbe  wa mabaraza ya Katiba wanaokuja kwenye mikutano na matamko ama nyaraka za vyama, badala ya maoni ya wananchi waliowachagua
Jaji alitoa kauli hiyo hiyo nzito wakati akifungua mkutano wa baraza la katiba katika Halmashauri ya Musoma vijijini muda mfupi baada ya kundi la tatu kuwasilisha maoni yake.
Kauli ya Jaji Wariona ilikuja mara baada ya mjumbe Tobias Maugo kuchangia maoni kwenye rasimu ya Katiba akitumia waraka unaodaiwa kusambazwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wanachama wake kikiwataka washinikize kupitishwa kwa mapendekezo ya chama hicho
Mjumbe huyo alikuwa akiusoma waraka huo neno kwa neno kana kwamba ilikuwa maoni yake mwenyewe.
“Mjumbe unasoma waraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao sisi Tume tayari tunao mikononi mwetu. Hatukuzuia kusoma tena lakini nilitaka tu kukwambia kuwa kama una maoni mengine, uyasema kwa kuwa waraka huo tunao tayari.’’
Waraka wa CCM kwa wanachama wake umeanza kuleta tafrani ambapo juzi mkoani Iringa Mjumbe wa Tume ya Katiba alimzuia mmoja wa wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya kutumia waraka huo kutoa maoni yake.
Alhaj Said El-Maamry ambaye kitaalamu ni mwanasheria, alimzuia Hussein Kiswil aliyekuwa akichangia mapendekezo kwenye rasimu hiyo, baada ya kubaini kuwa, alichokuwa anazungumza kilitokana na maelekezo ya CCM.
Hata hivyo hatua hiyo ilizua tafrani katika mkutano huo, baada ya mjumbe huyo wa Baraza la Katiba wilaya, kutoridhika na msimamo huo wa mjumbe wa tume na kupendekeza afukuzwe kwenye mchakato huo, kwa kile alichoeleza kuwa anapingana na maelekezo ya kuwaacha watu watoe maoni yao kwa uhuru.
Kiswil alidai kuwa mjumbe huyo hastahili kuendelea na kazi ya kusimamia mabaraza hayo kwa kuwa yeye pamoja na wajumbe wenzake kadhaa, hawana imani naye.
“Siku ya jana (juzi) tukiwa ndani ya ukumbi huu mlitueleza kuwa kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake katika kuchangia rasimu ya katiba hii, mimi nilichaguliwa kuingia katika kundi na kupewa jukumu la kuchambua muundo Muungano” alisema Kiswil na kuongeza;
“Nilipoanza kuchangia mimi aliingia Mjumbe wa tume El-Maamry na kusikiliza, nilipomaliza kabla hata ya kuruhusiwa na mwenyekiti alianza kuzungumza akisema maoni niliyotoa mimi ni maelekezo ya chama cha Mapinduzi na aliongeza kuwa ana taarifa za kuwapo kwa kiongozi mkubwa wa kisiasa aliyekuja Iringa kutoa semina… Nilitaka anithibitishie kama hayo aliyoyasema ni ya kweli.”
Kitendo cha CCM kuusambaza waraka huo kwa wanachama wake kinaelezwa kuwa ni kinyume na kanuni na utaratibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka watu watoe maoni yao wenyewe.
Tayari baadhi ya wajumbe wa Mabaraza ya Katika ngazi ya wilaya waliopata waraka huo wameripotiwa kuanza kuutumia kujenga hoja katika mijadala inayoendelea maeneo mbalimbali nchini.

1 comment:

  1. when it come a time nothing can prevent

    ReplyDelete