Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kunasa waraka wa siri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaokwenda kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, ukimshinikiza kukubali mapendekezo yao.
Waraka huo wa CCM uliosainiwa na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Jitu Vrajilal Soni una lengo la kupinga mapendekezo mbalimbali yaliyomo katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya iliyozinduliwa Juni 3 mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Mashariki na Pwani, Mabere Marando akihutubia mkutano wa chama hicho uliofanyika katika viwanja cha Shule ya Msingi Ukombozi, Manzese jijini jana alidai waraka huo una lengo la kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya yenye manufaa kwa Watanzania wote.
Marando akisoma baadhi ya mapendekezo ya CCM yaliyomo katika waraka huo kwenda kwa Jaji Warioba kumtaka kuviondoa vipengele vilivyomo ndani ya Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya vinavyohusu Tunu ya Taifa, kuwa bila kufanya hivyo hakutakuwa na tija ya uwajibikaji.
Alizitaja tunu hizo za taifa kuwa ni kuwa utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa ambazo Chadema wanaziunga mkono zipite na kuwa sheria.
“Sisi Chadema tunaona zinafaa kutokana na umuhimu wake lakini CCM wamemwambia Warioba aondoe neno uwazi wakiwa na maana ya kuwa wanataka mambo yao yasiwekwe wazi,” alisema Marando.
Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho alisema, Jaji Warioba amependekeza utajiri wa taifa uendelezwe na kuzuia mtu kumnyonya mwenzake jambo ambalo CCM wamelipinga.
“CCM katika waraka huo ibara ya 11.2 na 11.3 wamemwambia Warioba viondolewe, sasa viongozi wa CCM na Chadema ni kina nani wanawapenda wananchi wake,” aliwauliza wananchi waliojitokeza katika mkutano huo na kujibiwa na kelele kuwa ni Chadema.
Marando alisema katika kipengele cha maadili ya taifa na jamii kinachosema viongozi wanatakiwa kuzingatia uongozi, utoaji wa huduma, kufanya usawa na kupiga vita rushwa mapendekezo ambayo yakipita kuwa sheria yatasaidia kupunguza tatizo la rushwa la utoaji wa huduma uliotukuta.
“CCM ambao hawaonyeshi dhamira ya kumkomboa mwananchi wake, wamemwambia Warioba kuyaondoa maadili hayo kwani hayafai, sasa kupiga watu, kula rushwa kweli liondolewe? Hawa CCM kweli hawataki tupate katiba ya kuwakomboa wananchi,” alisema Marando na kuongeza:
“Kama hiyo haitoshi wamesema kitendo cha wananchi kumwajibisha mbunge wao kama hatakuwa anatimiza majukumu yake nao wamesema mapendekezo hayo hayafai. Kweli CCM hawataki tupate Katiba Mpya.”
No comments:
Post a Comment