Sunday, June 2, 2013

Warioba amnusuru JK

TUME ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kutangaza wakati wowote kuanzia kesho rasimu ya Katiba Mpya, iliyosheheni mambo mazito yaliyoelezwa kuwa yatamnusuru Rais Jakaya Kikwete katika lawama zitokazo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Habari za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali zimesema kuwa rasimu hiyo imejaa mapendekezo mengi mazuri ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele na kuumiza vichwa vya watawala na Watanzania wengi.
Taarifa zimebainisha kuwa wajumbe wa tume hiyo chini ya uongozi wa Jaji mstaafu, Joseph Warioba, wamesoma upepo, wakaweka kando itikadi za kisiasa na kutanguliza masilahi ya nchi.
Moja ya mambo mazito yaliyopendekezwa katika rasimu hiyo ni mfumo wa muungano. Taarifa zinasema tume imezingatia matakwa ya wakati, na madai ya muda mrefu kupitia majukwaa, vyombo vya habari na hata tume za majaji Francis Nyalali na Robert Kisanga, kuhusu mfumo wa muungano. Imependekeza kuundwa kwa serikali tatu kama suluhisho la mizozo iliyopo.
Ukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wadai wengi waliojadili mfumo wa muungano wamekuwa wakipendekeza serikali tatu. CCM wanataka ziendelee kuwa mbili za sasa.
Pendekezo jingine kubwa ambalo limezingatiwa na wajumbe wa tume hiyo na ambalo limekuwa likipigwa danadana kwa miaka mingi ni kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi.
Itakumbukwa kwamba, suala la kutaka kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi kama ilivyo kwa lile la muungano, limepigiwa kelele kwa muda mrefu na vyama vyote vya upinzani ambavyo vimekuwa vikilalamika kutotendewa haki katika chaguzi mbalimbali zilizopita.
Vyama vyote, ikiwamo CCM, vimependekeza tume huru ya uchaguzi, ingawa kichinichini, makada wengi wa CCM na viongozi, wanadai tume ikiwa huru wataondoka madarakani.
Baadhi yao ni wale wanaoendelea kumlaumu Rais Kikwete kuruhusu mchakato wa Katiba mpya ambao ulikuwa ajenda ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Kama itakuwa huru, Tume ya Uchaguzi itaondoka chini ya kivuli cha rais, ambaye amekuwa akipendekeza na kuteua wajumbe, ambao pia wanawajibika kwake. Mtindo huu umekuwa ukikipendelea chama tawala.
Mambo mengine mazito yaliyomo ndani ya rasimu hiyo ni suala la umri wa mgombea wa nafasi ya urais. Tume katika rasimu hiyo inataka umri wa mgombea urais uwe miaka 40 na zaidi, kama ilivyo sasa.
Kadhalika, tume imependekeza kufutwa rasmi dhana ya ujamaa na kujitegemea katika katiba. Badala yake, inapendekeza katiba itamke kuwa Tanzania itakuwa nchi ya demokrasia na kujitegemea.
Pendekezo jingine ni kwamba mawaziri hawatakuwa wabunge, ili kutenganisha majukumu ya kiserikali na kibunge, kama ilivyopendekezwa na wadau wengi.
Kwa mapendekezo hayo na mengine, Tume imemwokoa Rais Kikwete ambaye amekuwa akilaumiwa kwa kukiuka makubaliano kati yake na CHADEMA kuhusu mabadiliko ya sheria inayosimamia mchakato huu.
Katika makubaliano hayo, CHADEMA na Kikwete walikubaliana kubadili sheria hatua kwa hatua ili kutengeneza mazingira mwafaka yatakayoleta katiba mpya inayotarajiwa, yenye kuleta matumaini ya kujenga na kuaminiana na mwafaka wa kitaifa; kwani kwa sheria ilivyo sasa, mchakato huu umehodhiwa na CCM na rais mwenyewe.
Ilikubaliwa kwamba kungekuwapo na mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo hatua kwa hatua bungeni.
Hata hivyo, baada ya kufanya marekebisho ya kwanza juu ya muundo wa Tume ya Katiba, serikali imegoma kupeleka muswada wa marekebisho mengine kama ilivyokuwa imekubaliwa kati ya Rais Kikwete na CHADEMA.
Katika siku za hivi karibuni, CHADEMA walitishia kujiondoa katika mchakato huo iwapo mambo kadhaa yasingetimizwa kabla ya mwisho wa Bunge la bajeti linaloendelea.
Katika taarifa ya wiki iliyopita, CHADEMA kilisema: “Endapo hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho serikali itakuwa haijaleta muswada wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya; basi CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha umma kukataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo mbovu.”
Duru za kisiasa ndani ya CCM zinasema hatua ya CHADEMA kususia mchakato huu imekuwa inawatia homa viongozi wakuu wa chama tawala kwa kuwa inaweza kuathiri mwelekeo wa wahisani, ambao watawala wasingependa kuwaudhi.
Hatua yoyote ya Tume ya Katiba kuleta rasimu yenye kukidhi matarajio ya wengi, itakuwa faraja kubwa kwa Rais Kikwete binafsi, ambaye amekuwa akizongwa na CCM kwa hatua yake ya kukaa na CHADEMA na kukubali kurekebisha sheria na kwa upande mwingine anazongwa na CHADEMA kwa usaliti aliowafanyia baada ya makubaliano tangu Novemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment