Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Dk Willbroad Slaa amesema ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji kwa viongozi umechangia kushindikana kuchukuliwa maamuzi magumu.
Alitoa mfano wa baadhi ya viongozi kutajwa kujihusisha na utoroshaji na uuzaji wa maliasili za nchi yakiwemo madini ya aina mbalimbali huku nchini ikiendelea kubaki masikini.
Dk. Slaa alisema hayo wakati wa mahafali ya Umoja wa wanafunzi wa Vyuo vikuu ambao ni wanachama wa chama hicho (Chaso) mkoani Morogoro na kuwatunuku vyeti vya chama hicho kwa kuthamini mchango wao wa kuendeleza Chadema wakati wakiwa katika vyuo hivyo.
Alisema kuwa hivi sasa Taifa limefikia pabaya kila kona kutokana na viongozi hao kila mtu kwa wakati wake kujichukulia chake mapema na kusababisha nchi kuendelea kuwa masikini.
Alitoa mfano baadhi ya viongozi hivi karibuni kushindwa mpaka sasa kuchukuliwa hatua kutokana na tuhuma za kuhujumu maliasili za Taifa.
Alisema kuwa ili suala la uadilifu liwepo ni lazima wanafunzi hao waliohitimu vyuo vikuu wahakikishe wanakwenda katika kazi zao kujenga uaminifu na uadilifu mkubwa ili kurudisha imani kwa wananchi.
Hata hivyo, Dk Slaa aliponda suala la kupiga marufuku kuzungumzwa kwa masuala ya kisiasa katika vyuo vikuu kuwa ni sawa na mawazo mgando kwa kuwa viongozi wanaotegemewa kuongoza baadaye watatoka katika vyuo vikuu.
No comments:
Post a Comment