RASIMU ya Katiba mpya yenye ibara 240 imezinduliwa jana huku Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu, Joseph Warioba, akiweka wazi kuwa imezingatia mawazo mapana ya wananchi wengi waliotoa maoni.
Kwa mujibu wa Warioba katika rasimu hiyo vipengele vingi vinavyotoa fursa kubwa ya kuruhusu mabadiliko yatakayochangia ustawi na maendeleo ya Watanzania.
Tunaamini mapendekezo mengi yaliyo kwenye rasimu yatachangia kuboresha umoja, mshikamano na utulivu vilivyojengeka kwa muda mrefu.
Rasimu hiyo imejaribu kujibu kilio cha Watanzania wengi ambao mara kwa mara wamekuwa wakilalamikia Katiba iliyopo hivi sasa haiendani na mabadiliko yanayotokea kila kukicha yakiwemo ya kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia.
Tumefarijika kuona rasimu hiyo imeruhusu mgombea binafsi, matokeo ya Rais kuhojiwa mahakamani, Spika na naibu wake wasitokane na vyama, mawaziri wasiwe wabunge na mengine mengi ambayo kama yataridhiwa na wananchi yataleta mabadiliko makubwa sana.
Rasimu hiyo pia imependekeza idadi ya mawaziri na wabunge ipungue ili kuboresha ufanisi pamoja na kupunguza gharama zinazolalamikiwa kila uchao.
Tunaamini wananchi na viongozi wote watakaohusika katika mchakato wa kuelekea kupata Katiba mpya watajikita kujadili masuala muhimu yenye mwelekeo wa kujenga taifa bila kujali itikadi za vyama.
Itikadi za vyama kamwe haziwezi kulisaidia taifa letu, vyama huzaliwa na kufa lakini taifa halifi hivyo ni vema kila mmoja wetu akashiriki kikamilifu kwenye zoezi la kura za maoni ili Katiba mpya ipatikane pasi na vurugu.
Tunaamini Tanzania itaiga mfano mzuri wa Kenya iliyoandika Katiba mpya iliyotumika katika uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni bila kufanya vurugu.
Hakuna sababu kwa Watanzania kushindwa kuandika Katiba mpya bila vurugu, hii ni fursa adhimu na ni vema sisi sote tukaitumia ili iwe mfano kwa mataifa ya nje.
No comments:
Post a Comment