Jana Tume ya Katiba Mpya iliwasilisha rasimu ya katiba hiyo ambayo sasa itapelekwa kwa wananchi kujadiliwa katika mabaraza ya katiba.
Rasimu hiyo iliwasilishwa kwa umahiri mkubwa na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.
Tunasema kuwa kilichofanywa jana na Tume hiyo ni kuandika historia. Kwa yeyote ambaye alikuwa anafuatilia kwa karibu hotuba ya Jaji Warioba katika kuwasilisha rasimu hiyo, atakubaliana nasi kwamba huu ni mwanzo mzuri wa kuipeleka Tanzania kuwa na katiba ya kisasa inayoakisi mahitaji ya sasa ya wananchi wake na siku zijazo.
Tunasema kutoka sakafu za mioyo yetu kwamba kazi nzuri imefanywa.
Tunapongeza ujasiri wa Tume ya Katiba kwanza kwa kutambua kuwa kila zama zina vitabu vyake, imethubutu kupendekeza mambo ambayo huko nyuma yalikuwa kama mwiko kiguswa, kutamkwa au hata kudadisiwa. Hapa tunalenga masuala la Muungano na hata madaraka ya rais.
Tume imetoa pendekezo la kuanzishwa muundo mpya wa Muungano kuwa wa serikali tatu, kwa maana ya serikali ya Shirikisho, ya Tanzania Bara na ya Zanzibar.
Jaji Warioba alisema kazi ya kufikia uamuzi huo haikuwa rahisi kwa sababu katika maoni mbalimbali yaliyotolewa na wananchi, wapo waliokuwa wanataka Muungano wa serikali moja, serikali nne, kuendelea na muundo wa sasa wa serikali mbili na pia walikuwako wa Muungano wa mkataba.
Alisema kimsingi sheria iliitaka Tume kuzingatia uwapo wa Muungano. Kwa hiyo hawakuchukua maoni ambayo yanataka kuvunja Muungano ingawa yalikuwa ya watu wachache.
Bonyeza Read More Kuendelea
Alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, walifanya rejea ya mapendekezo na maandiko mbalimbali, kutazama uzoefu wa mataifa mengine, lakini pia kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali na Jaji Robert Kisanga.
Tume zote zilipendekeza kuwako kwa Muungano wa serikali tatu.
Katika kushughulikia Muungano, Jaji Warioba pia alisema kuwa orodha ya mambo ya Muungano yamepunguzwa kutoka 22 hadi saba.
Aliorodhesha mambo saba ya Muungano ambayo ndiyo yatapelekwa kwa wananchi ili kutolewa maamuzi, kuwa ni Katiba, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyokuwa ya kodi.
Katika mapendekezo hayo pia muundo wa Bunge la Muungano nao umeguswa na sasa litakuwa na viti 75 tu, kwa uwiano wa wabunge kutoka Tanzania Bara 50 na Zanzibar 20, huku wabunge watano wakiwa ni wa kuteuliwa na Rais kutoka kundi la walemavu.
Viti maalum vinafutwa na badala yake kila jimbo la uchaguzi litakuwa na wabunge wawili, mmoja mwanamume na mwingine mwanamke, hali ambayo itasaidia kuleta usawa wa kijinsia.
Rasimu pia imejikita kupungaza gharama za kundesha serikali kwa kupunguza idadi ya majimbo ya uchaguzi ambayo yatakuwa ni 25 kwa Tanzania Bara na Zanzibar 10 tu, idadi ya mawaziri nayo imewekewa ukomo kikatiba kuwa 15 tu.
Rasimu inaongeza madaraka kwa wananchi kuwadhibiti wabunge wao, kwa kuanisha mfumo wa kuwaondoa madarakani kama hawatimiza wajibu wao, kuhoji matokeo ya urais, kuanzisha fursa ya wagombea binafsi, kulinda kiti cha Spika kisitumike kisiasa kwa Spika na naibu wake kutokuwa wabunge au kushika nafasi za uongozi wa kisiasa katika vyama vya siasa.
Tume hiyo pia inapendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ambayo pia itachukua majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na wajumbe wake sasa watatokana na sifa za kikatiba na watateuliwa na kamati ya uteuzi na kuthibitishwa na Bunge.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Katiba inapendeza kuwa na misingi mingi na tunu za taifa, huku dira ya taifa nayo ikiwekwa kikatiba kwa maana kwamba kiongozi yeyote ambaye ataingia madarakani atawajibika kutekeleza na kusimamia dira hiyo.
Kimsingi kila tukitazama kazi iliyofanywa na Tume ya Katiba tunapata faraja kwamba kwa kiwango cha juu kabisa imetoa mapendekezo mazuri na mazito ambayo siyo tu yanakidhi kiu ya wananchi wengi, bali pia yanatoa picha kwamba kimsingi Tanzania itapata katiba mpya nzuri kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Tunaamini kwamba kwa mwanzo huu, Tume iko katika mstari wake, na kwa ushirikiano wa wananchi, na kwa utaratibu mzuri katika mijadala kwenye mabaraza ya katiba, mwisho katiba nzuri itapatakana na hivyo kuifanya Tanzania kuendelea kuwa na sifa ya kufanya mambo yake kwa amani, utulivu na kufikia mwisho mwema bila kuparaganyika.
No comments:
Post a Comment