ZITTO: KUHUSU UMRI NAHESHIMU UAMUZI
MWENYEKITI wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Deus Kibamba, ameipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuandaa rasimu iliyogusa mambo muhumu kwa maslahi ya taifa.
Pamoja na Kibamba, wengine walioipongeza tume hiyo ni wabunge, wanasiasa na wanaharakati ambao walizungumza na Tanzania Daima kwenye viwanja vya Karimjee muda mfupi baada ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba kuitangaza Rasimu ya Katiba mpya.
“Kwa kweli naipongeza tume; zipo kasoro kidogo za hapa na pale lakini kwa ujumla wake wamefanya kazi nzuri inayostahili pongezi,” alisema Kibamba.
Kuhusu hofu ya JUKATA kwamba muda wa kupata Katiba mpya ulikuwa hautoshi, alisema muda uliobaki ukitumika vema utatosha na kusisitiza kwamba ifikapo Aprili mwakani taifa litakuwa na Katiba mpya iliyo bora.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA) alisema Rasimu ya Katiba imeshindwa kugusa biashara ya kimataifa kwa kuiondoa nje ya masuala ya Muungano.
Kwa mujibu wa Zitto dosari hiyo inaweza kufanyiwa mabadiliko kwenye mabaraza na Bunge la Katiba huku akiipongeza Tume ya Jaji Warioba.
“Wazee wetu wamefanya kazi; wamejitahidi kadiri ya uwezo wao. Kuna maeneo hasa masuala ya Muungano wamefanya vizuri, kuwaondoa wabunge kuwa mawaziri kutaongeza uwajibikaji.
“…Suala la kimapinduzi ni lile la wananchi kuwaondoa wabunge wao ambao hawafanyi kazi vizuri kwa hiyo badala ya kusubiri miaka mitano wanaweza kumwondoa wakati wowote; hili ni jambo jema tunalotakiwa kuliendeleza,” alisema.
Kuhusu umri wa mgombe urais kuanzia miaka 40 Zitto ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara kwa CHADEMA, alisema anaheshimu uamuzi wa tume hiyo.
Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema rasimu hiyo inatoa uwanja mpana kwa wananchi kushiriki kwenye uendeshaji wa nchi.
“Idadi ya washiriki wa wanawake itaongezeka kwenye Bunge la Muungano… changamoto zipo hasa linapokuja suala la mabadiliko ambayo ni lazima yafanyike ila nahitaji muda zaidi kuisoma rasimu hii kwa kina.
“…Sababu za uwepo wa mgombea binafsi ni kuimarisha ushiriki wa wananchi moja kwa moja katika uendeshaji wa serikali yao,” alisema Dk. Migiro ambaye ni Katibu wa Halmashauri ya Chama cha Mapinduzi (NEC-CCM) anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Kwa upande wake waziri mkuu wa zamani, Dk. Salim Ahmed Salim, alisema kutangazwa kwa rasimu hiyo kunaonyesha mwanga wa Katiba bora ya Tanzania inayozingatia Muungano.
No comments:
Post a Comment