Saturday, June 8, 2013

Si sawa CCM kuunda ‘jeshi’ lake

KATIKA toleo la leo, tumechapisha habari zinazokituhumu Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mbeya, kuanzisha kambi maalumu inayodaiwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wa chama hicho.
Tuhuma hizo ambazo pia zimethibitishwa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani, zinasema kuwa kuanzishwa kwa kambi na mafunzo hayo kunatokana na maagizo ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba.
Haya yanatokea kukiwa na kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika baadhi ya mikoa, ukiwemo wa Mbeya na Arusha ambako tayari kumeripotiwa kutokea kwa matukio ya kikatili ya kushambuliwa vibaya kwa baadhi ya wafuasi wa CHADEMA.
Sio mara ya kwanza kwa Watanzania kuambiwa kuwepo kwa kambi za vijana wanaowekwa kambini na Chama cha Mapinduzi; mwaka juzi tulishuhudia kambi ya vijana katika kijiji cha Ulemo, jimbo la Iramba Magharibi, anakotoka Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Ni yeye aliyeweka bayana kuwa kulikuwa na vijana 384 wa CCM waliokuwa wanapata mafunzo kwa kile kinachoitwa kuwaongezea morali ya kukitetea chama.
Hatuungi mkono hatua hiyo ya chama kuandaa vijana kwa ajili ya uchaguzi kwani nchi yetu kwa mujibu wa sheria uchaguzi unalindwa na jeshi la polisi ndilo lenye jukumu la kulinda raia.
Hatua ya Chama cha Mapinduzi kuweka vijana kambini kuwapa mafunzo ya kijeshi kila kunapokuwa na uchaguzi haileti picha nzuri katika jamii; lakini pia inaweza kuchochea machafuko ambayo mwisho wake huleta maafa.
Tumepokea kwa mshtuko mkubwa kauli ya kamanda wa polisi mkoani humo kuwa “kambi hiyo imeanzishwa kwa maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi”.
Ni hatari kwa usalama wa nchi yetu kwa jeshi la polisi kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi ili kuruhusu vikundi vya wafuasi wa vyama kupewa mafunzo ya kijeshi.
Tunatoa wito kwa jeshi la polisi ambalo kazi yake ni kusimamia usalama wa ndani ya nchi na kuwashauri viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuvunja kambi hiyo kwani iko kinyume cha sheria na inachochea uvunjifu wa amani nyakati za uchaguzi.
Tuna hakika kila chama kina uwezo wa kuwa na vikundi kwa ajili ya kujilinda nyakati za uchaguzi, lakini tukiweza kuruhusu suala hilo tunaingiza nchi yetu katika machafuko bila sababu za msingi; tukubaliane na jeshi la polisi lililopo kuwa linatosha kuwalinda raia wake na kusimamia haki, kwa hiyo kama jeshi limeanza kuingiliwa na Chama cha Mapinduzi kuruhusu vitu kama hivyo kutokea bila kuchukua hatua, yaweza kuwa sababu mojawapo ambayo hutolewa kila mara na vyama vya upinzani kuwa jeshi la polisi linatumiwa vibaya na chama tawala.
Matukio mbalimbalu yameripotiwa ya kutishiwa wafuasi wa vyama vya upinzani kwa bastola au wengine kujeruhiwa; mathalani juzi imeripotiwa matukio kama hayo kutokea katika jiji la Arusha ambako pia kampeni zinaendelea.
Tunalishauri jeshi la polisi kusaidia watu wafuate sheria pasipo shuruti na lionyeshe kuwa lenyewe ndilo lina wajibu wa kulinda raia, sio kuruhusu  vyama vya siasa kujiundia majeshi kadiri ya mahitaji yao.
Hali hiyo ni hatari na hatudhani kuwa jeshi la polisi limeshindwa kuidhibiti vinginevyo usalama wa raia na siasa ya nchi yetu vitakuwa vitakuwa katika mtikisiko mkubwa.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment