JUMLA ya sh bilioni 4.24 zinakadiriwa kutumika katika kutekeleza miradi yote ya umeme katika wilaya Karatu pamoja na kuwaunganishia nishati hiyo wateja wa awali wapatao 1217.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (CHADEMA).
Mbunge huyo alitaka kuelewa ni lini serikali itapeleka umeme Mang’ola ili kuwawezesha wananchi kunufaika na kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Eyasi.
“Serikali ilishatoa tathmini ya awali ya gharama ya kupeleka umeme Mang’ola kiasi cha sh bilion 1.1 na tathmini ya kupeleka umeme Mbulu kupitia mradi wa REA pia ilishafanyika; je, ni lini serikali itapeleka umeme kule Mbulumbulu?” alihoji Natse.
Akijibu swali hilo, Masele alisema kuwa serikali kupitia kwa wakala wa nishati vijijini itatekeleza mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya Mang’ola na Mbulumbulu ikihusisha vijiji vyote vitakavyopitiwa na nishati huyo.
Alisema kuwa zabuni ya kazi hiyo ilikwishatangazwa na sasa uchambuzi wa kupata mkandarasi unaendelea ili kazi hiyo ianze kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha.
Aliainisha kuwa gharama za kutekeleza miradi yote katika wilaya ya Karatu zinakadiriwa kuwa ni sh bilioni 4.24 na kuwaunganishia wateja wa awali wapatao 1217.
No comments:
Post a Comment